Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) imeendelea kusisitiza nafasi yake kama kinara wa huduma za kidijitali nchini kwa kuzawadia wateja wake kupitia kampeni maalum ya Mahaba Kisiwani. Kampeni hii imewahusisha wateja waliofanya miamala mingi zaidi ya kidijitali, wakijishindia safari ya kifahari ya kwenda Zanzibar na malazi ya bure.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Februari 14, Mkurugenzi wa Biashara wa Wateja Wadogo, Lilian Mtali, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCB, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 ya ubora wa huduma za benki hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Mtali alisema kuwa kampeni ya Mahaba Kisiwani ni mfano wa juhudi za kimkakati za benki hiyo katika kukuza matumizi ya teknolojia za kidijitali kwa wateja wake.
“Kwa kuwazawadia wateja, tunapanua wigo wa utoaji wa huduma kwa njia za kidijitali ambazo ni salama, rahisi na zenye ufanisi zaidi. Hii ni njia bora ya kuwahamasisha wateja wetu kutumia teknolojia hizi za kisasa,” alisema Mtali.
Akiendelea kufafanua, aliongeza kuwa kampeni hii ililenga kuwapa motisha wateja wa benki hiyo kufanya miamala ya kidijitali huku wakijiongezea nafasi ya kushinda safari ya kwenda Zanzibar kwa mapumziko ya wikiendi.
Aidha, Mtali alitoa pongezi kwa wateja na wafanyakazi wa TCB kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 100.
“Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja. Tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi, kuhakikisha kila mmoja anathaminiwa, na kuimarisha huduma bora kwa wateja wetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Kidijitali na Ubunifu, Jesse Jackson, alihimiza wateja wote kuendelea kutumia huduma za kidijitali kwa urahisi wa kupata huduma bila kufika matawini.
“Huduma za kidijitali sio tu zinapunguza muda wa kufika benki, bali pia zinawapa wateja ufanisi na usalama wa hali ya juu katika kufanya miamala yao ya kila siku,” alisema Jackson.
Benki ya TCB, ikiwa na historia ya miaka 100 ya utoaji wa huduma bora, inaendelea kuwa mfano wa ubunifu na ushindani katika sekta ya kibenki nchini.