Chato, Geita
Wananchi wa vijiji vya Imweru, Mulanda, Kibumba na Buseresere wilayani Chato mkoani Geita wamenufaika na ujenzi wa boksi kalavati na kuchongewa barabara yenye urefu wa Km 8 barabara ya Mulanda – Imweru ambapo hapo awali kulikuwa ni vikwazo katika kuvuka eneo hilo hasa kipindi cha masika.
Meneja wa TARURA wilaya ya Chato, Mhandisi Ernest Nyanda amesema kuwa barabara hiyo inasaidia kuzifikia huduma za kiutawala, kijamii na shughuli za kilimo.
“Kipindi cha mvua ilikuwa ni vigumu kwa wanafunzi kuvuka hapa, huduma za elimu pamoja na afya zilipatikana kwa shida, ndio maana ikapelekea mradi huu wa uondoaji vikwazo katika barabara (Bottleneck) ukaelekezwa kwenye barabara hii”, amesema.
Naye, Bw. Semeni Marko ambaye ni mkazi wa kijiji cha Buseresere amesema kuwa eneo hilo lilikuwa korofi na hawakuweza kupita wakati wa masika ambapo wanafunzi walikuwa wanashindwa kwenda shuleni, lakini sasa wanafika shuleni bila shida.
Naye, Bw. Yote Marko, mkazi wa Kijiji cha Imweru, ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kuondoa vikwazo katika barabara hiyo na kuwawezesha wananchi wa makundi mbalimbali kuvuka kwa urahisi.
Mradi huo wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia umehusisha ujenzi wa boksi kalavati pamoja na kuchonga barabara yenye urefu wa km 8 na kuweka changarawe ili ipitike kwa kipindi chote cha mwaka.