Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akifunga mkutano huo mkoani Arusha leo.



Washiriki mbalimbali wa mkutano huo wakifuatilia mada wakati wa kufunga mkutano huo mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro, Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (Mb) amesema kuwa ,Serikali imedhamiria kuimarisha na kuongeza matumizi ya TEHAMA ili kwenda sambamba na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa shughuli nyingi duniani ikiwemo za kiuchumi kwa sasa zinafanyika kwa kutumia TEHAMA.
Simbachawene amesema kuwa,Serikali imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA, hususan katika masuala ya utafiti na ubunifu, ili kuimarisha usalama wa Mtandao wa Mawasiliano na kuongeza watumiaji wa internet.
Hata hivyo amezitaka Taasisi za Umma ambazo bado zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA ili kuleta tija katika utendaji kazi wao.
Ameyasema hayo leo wakati wa kufunga Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao kilichofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa AICC jijini Arusha na kuhudhuriwa na wadau takribani 1500 wakiwemo Maafisa Masuuli, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA, Maafisa TEHAMA na watumiaji wengine wa mifumo ya TEHAMA kutoka katika Taasisi, Halmashauri na Mashirika mbalimbali ya Umma.
Ameongeza kuwa,Wizara kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), imejipanga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma mtandao kwa umma kidijitali sambamba na kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima, ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma kwa wakati na kwa gharama kupitia mifumo ya TEHAMA.
‘Tunajivunia kuona idadi ya watumiaji wa simu za mkononi pamoja na internet, inaongezeka mwaka hadi mwaka. Ongezeko hili linatupa chachu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi na linadhihirisha ongezeko la matumizi ya TEHAMA hapa nchini.” ameongeza Waziri.
Waziri Simbachawene amezitaka taasisi za umma kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha zinatumia fursa ya ongezeko hili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kidijitali kupitia simu za mkononi.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Mulula Mahendeka amesema Vikao vinavyofanyika vimekuwa na manufaa makubwa katika kukuza na kuendeleza jitihada za Serikali Mtandao, kupitia mawazo mbalimbali yanayotolewa na washiriki wa vikao.
Mahandeka amesema Wizara, itasimamia utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa kwenye kikao hiki kwa wakati, ikiwa ni kwa Wizara yenyewe, e-GA au taasisi nyingine ya umma inayohusika.
Kwa upande wake ,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Benedict Ndomba amewashukuru washiriki wote kwa umakini, utulivu na usikivu walioonyesha wakati wote wa kikao, hali ambayo imechangia kupata mawazo bora wakati wa majadiliano.
Amesema mawazo yaliyotolewa ni chachu katika maendeleo ya Serikali Mtandao, na Mamlaka itayafanyia kazi maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa kwa kuwa na jitihada za Serikali Mtandao zenye tija zaidi.
Ndomba amesema mawazo jumuishi katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao ni chachu ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi kidijitali, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hizo kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu.