……………..
Na Saidi Lufune – Arusha
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba amesema Wahasibu wa Wizara hiyo na Taasisi zake ni chachu na nguzo muhimu ya kufanikisha malengo ya Wizara na Serikali kwa ujumla, kutokana na jukumu la ukusanyaji, usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma
CP. Wakulyamba ameyasema hayo leo Februari 13, 2025 Jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo wahasibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake ambapo amesema licha ya mafunzo hayo kuwaongezea uwezo pia yatawasaidia katika kuwaongezea ujuzi na maarifa ya usimamizi wa mambo ya fedha katika Taasisi na Wizara kwa ujumla
“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yatakua endelevu kila mwaka ili kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao na kupelekea kufanikisha matarajio ya serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mbeba maono makubwa katika kukuza sekta ya utalii kwa vitendo.” Amesema CP. Wakulyamba
Katika hatua nyingine C.P Wakulymba amewataka wahasibu wakuu wa Wizara hiyo na Taasisi zake kuwa washauri wazuri kwa viongozi wao ili kuepukana na changamoto za kikanuni za matakwa ya kifedha kulingana na miongozo kwa kubainisha mapungufu wakati wa ufungaji wa hesabu na kasoro katika kujibu hoja za ukaguzi wa ndani na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
“Sisi kama viongozi tunawategemea sana nyinyi ili tusiharibu, tunategemea ushauri wenu kwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu zaa fedha katika kusimamia matumizi ya Serikali” Amesema CP. Wakulyamba
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Paul Kabale amepongeza uongozi wa Wizara na wahasibu na Taasisi zake kwa kuendelea kupata hati safi kwa ukaguzi wa mwaka wa fedha 2022/2023 kutokana na usimamizi bora wa fedha za umma na makusanyo ya maduhuli ya serikali ndani ya wizara
“Na hii inatokana na ushirikiano na mahusiano mazuri baina yetu katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo uandaaji mzuri wa taarifa za fedha na hesabu za majumuisho na kujibu kwa ufasaha hoja za ukaguzi.” Amesema Kabale
Wakizungumza nje ya kikao hicho baadhi ya washiriki wa kikao hicho licha ya kushukuru uongozi wa wizara hiyo kwa kuwapatia mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yatawaongezea uwezo mkubwa katika usimamizi wa fedha na kuwa washauri wazuri kwa viongozi wao katika usimamizi wa fedha za umma na uwekezaji
Kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kimeendeshwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kikilenga kuwakumbusha wahasibu wa Wizara hiyo na Taasisi zake wajibu wao wa kuzingatia Sheria ya Fedha Sura Na.348 inayoelezea jukumu la usimamizi wa fedha za umma kwa lengo la kuhakikisha udhibiti na ufanisi