Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Bw. Fadhili Maganya akizungumza jambo katika Kikao na Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Ally Hapi akizungumza jambo katika Kikao na Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Dogo Mabrouk akisisitiza jambo katika Kikao na Wawekezaji Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Elimu, Malezi na Mazingira Wazazi CCM Taifa Dkt. Primus Mkwera akichangia mada katika Kikao na Wawekezaji Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Bi.Khadija Ally akizungumza jambo katika Kikao na Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na Vyuo Mbalimbali wakiwa katika kikao na uongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa kilichofanyika leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imejipanga kufanya maboresho makubwa ya uendeshaji wa Shule 71 zinazomilikiwa na Jumuiya hiyo kwa kuweka mkakati ya kuhakikisha shule hizo zinakuwa na viwango bora kwa kuingia ubia na wawekezaji ambao wataleta tija kwa kutoa huduma bora ya elimu.
Akizungumza leo Februari 12, 2025, Jijini Dar es Salaam katika Kikao na Wawekezaji katika Seka ya elimu wakiwemo wamiliki wa shule na vyuo Mbalimbali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Bw. Fadhili Maganya, amesema kuwa baadhi ya Shule za Jumuiya zimekuwa zikijiendesha kwa mafanikio, huku nyengine zikisuasua.
Bw. Maganya amesema kuwa ili kupata mafaniko wameona ni vizuri kukutana wawekezaji katika seka ya elimu ili kubainisha fursa zilizopo na kufanya kazi pamoja kwa njia ya ubia katika kuendesha shule hizo kwa makubaliano.
“Tumekutana na Bodi za Shule na Vyuo mbalimbali wakiwemo wanawake wawekezaji katika sekta ya elimu, wamiliki wa shule binafsi, Vyama vya Wakuu wa shule ambapo tumezungumza nao na kufungua milango ya kushirikiana kama tutakubaliana nao ” amesema Bw. Maganya.
Amefafanua kuwa kanuni za jumuiya ambazo zimetokana na katiba ya chama cha mapinduzi inawapa jukumu la kushughulika na elimu, hivyo kikao hicho na wadau wa sekta ya elimu ni sehemu ya kutafuta namna bora ya kuendesha shule za jumuiya, huku akiwakumbusha wawekezaji ambao wamepewa jukumu la kuendesha shule kuongeza ufanisi.
“Tofauti na uendeshaji wa shule, jumuiya ina mpango wa muda mfupi wa kufanya uwekezaji wa kuanzisha Hospitali ya rufaa pamoja na kujenga hospitali ya Mama na mtoto Pemba na hospitali nyingine Mkoani Iringa” amesema Bw. Maganya.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Ally Hapi, amesema kuwa ili kufikia malengo wanahitajika wawekezaji makini ambao wana uzoefu katika sekta ya elimu hasa kuendesha shule na vyuo.
Amesema kuwa kwa sasa jumuiya ya wazazi ina jumla ya shule 71, huku akieleza kuwa shule 18 zinaendeshwa Jumuiya ya wazazi , 18 nyingine zinaendeshwa na wabia na zlizobaki zimejifunga.
“Tunataka wawekezaji ambao wapo ‘serious’ sio ambao wanaokamata fursa ya kutumia rasilimali za jumuiya kutafuta fedha, wanahitajika wazoefu katika sekta ya elimu, wenye mtaji pamoja na aliyewahi kumiliki shule au vyuo” amesema Hapi.
Hapi amesema shule za jumuiya ya wazazi zipo Mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya ambapo kuna jumla ya Shule 16, Iringa zipo mbili, Songwe tano, Kigoma tatu, Ruvuma mbili, Tanga sita, Arusha moja, Njombe mbili , Kilimanjaro 10, Shinyanga tatu, Dar es Salaam nne pamoja na Morogoro mbili.
Mikoa mingine ni Simiyu mbili, Singida mbili, Mwanza moja, Katavi moja, Dodoma moja, Kaskazini Pemba moja, Kagera mbili, Mtwara mbili, Pwani moja na Chuo cha Kaole Bagamoyo, huku akieleza kuwa zipo taasisi zilizoonesha nia ya kuwekeza kwa mfano Chuo cha Mipango pamoja na Kanisa Katoliki.
Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Elimu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Bw. Robert Rwezaura amesema hatua hiyo ya ubia na wawekezaji anatarajiwa kuboresha utolewaji wa elimu nchini kwa shule zote zinazomilikiwa na jumuiya ya wazazi.