Diwani wa Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza Swila Dede akizungumza kwenye mkutano


Wananchi wa mitaa mitano iliyoko katika Kata ya Shibula wakiwa kwenye mkutano
……………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wananchi wa mitaa mitano iliyoko katika Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kutatua mgogoro wa mpaka mpya wa uwanja wa ndege na wananchi hao ndani ya siku saba ili waweze kujua hatima ya maisha yao.
Mgogoro huo uliodumu kwa miaka nane (8) umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kushindwa kuendeleza ujenzi wa makazi yao hivyo kupelekea watu wazima kulala nyumba moja na watoto wa kike na wakiume hatua inayosababisha kukosa amani ya ndoa kwa wazazi, pamoja na kuangukiwa na nyumba na kunyeshewa na mvua zenye upepo mkali.
Kutokana na changamoto hizo kamati pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa wameadhimia kwa pamoja kufanya mkutano ili kupaza sauti ya pamoja kwa Serikali yao na Dunia kwa ujumla ili waone mateso na manyanyaso makubwa yanayofanywa kwa wananchi wake.
Akizungumza kwenye mkutano huo Diwani wa Kata ya Shibula Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, Swila Dede amesema Serikali inapaswa kutambua maumivu ya wananchi wa kata hiyo kwani wamekuwa na maisha yenye mashaka kwakutokuwa na makazi bora.
Amesema makubaliano yao ya mwisho na viongozi ilikuwa ni wananchi kulipwa fidia na viongozi waliwahakikishia kuwalipa fidia lakini kwa sasa taarifa hiyo imebadilika na wamekuwa wavamizi wa eneo la uwanja wa ndege wa Mwanza jambo ambalo siyo halali.
“Wananchi wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu wanashindwa kuendelea ujenzi wanashindwa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo kujenga nyumba za wapangaji ambazo zingewasaidia kuongeza pato la familia hivyo ni vyema utatuzi huu ufanyike kwa haraka ili watu waweze kuendelea na maisha yao”, Amesema Dede
Akisoma taarifa fupi ya kamati ya ufatiriaji mgogoro huo, Katibu wa kamati hiyo Robert Luziri amesema mitaa mitano ya kata hiyo ambayo ni Mhonze “B”, Nyamwilolelwa,Kihili,Shibula na Bulyang’hulu kwa kushirikiana na wenye viti wa mitaa hiyo pamoja na diwani walikutana kupitia taarifa za uthamini iliofanyika Machi 27, 2024 hadi Mei 8, 2024.
Amesema katika kikao hicho walikubaliana maeneo yote yathaminiwe kwakuanza na ardhi,nyumba,misingi,maboma na vyote vilivyokwisha endelezwa pamoja na kupewa fomu namba moja baada ya uthamini kukamilika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kata hiyo wameeleza kuwa mgogoro huo umewapa wakati mgumu wa kushindwa kuendeleza maeneo yao huku wengine wakilazimika kukaa kwenye majumba mabovu.
“Tunaiomba Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu ituonee huruma kwani tunateseka sana sana hatuna makazi bora, tunalala chumba kimoja na watoto wetu ambao ni wakubwa hivyo tunaimani ndani ya hizi siku saba tutapata majibu ambayo yatakuwa na tija kwenye maisha yetu”, wamesema
Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela, Yusuph Bujiku amewasihi wananchi kuendelea kuwa watulivu katika suala hilo ambalo liko kwenye hatua mbalimbali za utatuzi.