Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Februari 12, 2025
Mkoa wa Pwani unatarajiwa kuwa na jumla ya vituo 1,913 vya kujiandikisha katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakalofanyika kuanzia Februari 13 hadi 19, mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la vituo 179 ikilinganishwa na 1,734 vilivyokuwepo mwaka 2019/2020.
Aidha, mkoa huo unatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 186,211, sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 992,067 walioko kwenye Daftari la Wapiga Kura, baada ya uandikishaji, mkoa utakuwa na jumla ya wapiga kura 1,178,278.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Suleiman Mtibora, alieleza Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ,inaendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, uzinduzi wa awali ulifanyika Mkoani Kigoma Julai 20, 2024, ambapo ulianzia katika mikoa ya Kigoma, Tabora, na Katavi.
Mtibora alieleza kuwa hadi Januari 16, 2025, Tume imekamilisha uboreshaji wa daftari katika mikoa 25, ikiwa ni pamoja na mikoa ya Kigoma, Tabora, na Katavi.
Aliongeza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuwa na jumla ya wapiga kura milioni 34.7, vituo 29,753 Tanzania Bara na visiwani Zanzibar 417, ambapo jumla ya vituo itakuwa 40,170.
“Watu 534,000 wanatarajiwa kutolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa sababu ya kukosa sifa, ikiwa ni pamoja na vifo, kutokuwa na akili timamu, na wale wanaotumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita,” alisema Mtibora.
Jaji (Rufaa) Mbarouk Mbarouk, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, alisisitiza kuwa mawakala au viongozi wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye vituo.
Kadhalika,viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia sheria ya Uchaguzi, kanuni za uboreshaji, na maelekezo ya Tume, huku wakiwa wanahakikisha kuwa miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji inazingatiwa.
Mbarouk alieleza kuwa, iwapo kutatokea changamoto yoyote, wadau wanapaswa kutumia taratibu zilizowekwa na sheria za uchaguzi ili kuzitatua. “Tume kwa upande wetu tutazingatia katiba, sheria ya Uchaguzi, na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hilo,” alisema.
Vilevile, Mbarouk alieleza kuwa kila chama cha siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura, Lengo la kutoa nakala hizo ni kuwawezesha vyama kupanga na kuweka mawakala wao katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.
Aliongeza kuwa, kila chama kitaruhusiwa kisheria kuwa na wakala mmoja kwenye kila kituo cha uandikishaji ili kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji na pia kuthibitisha sifa za wale wanaojiandikisha.
Kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024, uboreshaji wa daftari unahusu kuandikisha raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi au watakaotimiza umri huo kabla au wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na ambao hawajapoteza sifa chini ya sheria yoyote ya Uchaguzi.
Wakati huo huo, Ofisa Mwandikishaji wa jimbo la Kibaha Mjini, Dkt. Rogers Jacob Shemwelekwa, alieleza kuwa halmashauri ya Mji wa Kibaha itakuwa na jumla ya vituo 131 vya uandikishaji vitakavyokuwa kwenye Kata 14 na Mitaa yote 73.
Alitoa wito kwa waandikishaji wasaidizi wa ngazi ya jimbo na kata kuwa waadilifu na waaminifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao katika zoezi hili la kitaifa.
Dkt. Shemwelekwa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, alieleza mafunzo ya siku mbili waliyopatiwa waandikishaji hao yawe chachu ya utendaji kazi wao katika uboreshaji wa taarifa za wapiga kura na uandikishaji wapiga kura wapya.
“Jumla ya waandikishaji 262 kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha wamepatiwa mafunzo haya, na vituo 131 vitatumika katika zoezi hili, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu,” alisema Shemwelekwa.
Kaulimbiu za zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, 2025 ni: “Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora.”