Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka
2024, leo Februari 12, 2025.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakifuatilia
uchangiaji wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira wa Mwaka 2024, aliouwasilisha bungeni jijini Dodoma leo Februari
12, 2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi
Cyprian Luhemeja na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immaculate Semesi wakifuatilia kikao
cha Bunge wakati wa uwasilishaji na upitishaji wa Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024,
aliouwasilisha bungeni jijini Dodoma leo Februari 12, 2025.
………
Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria
ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024, leo
Februari 12, 2025 bungeni jijini Dodoma baada ya kufanyia marekebisho
kadhaa kutoka katika mapendekezo ya Serikali.
Akiwasilisha maelezo ya muswada huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Yusuf Masauni amesema lengo la
jumla la marekebisho yanayopendekezwa ni kuiwezesha Sheria hiyo kuendana
na Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na kutatua baadhi ya
changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Amesema Ibara ya 3 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu
cha 13 ambacho kinapendekezwa kurekebishwa ili kujumuisha masuala
yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika masuala ambayo
yanasimamiwa na Waziri.
”Madhumuni ya mapendekezo ya marekebisho hayo ni kumpa Waziri mamlaka
ya kudhibiti na kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Pia
kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya mazingira na
mabadiliko ya tabianchi anapata wasaa wa kutoa maoni yake kabla mipango
ya kitaifa ya maendeleo haijapitishwa na mamlaka husika,” amesema Mhandisi
Masauni.
Akiendelea, amesema kuwa Sehemu ya Tatu ya Sheria inapendekezewa
kurekebishwa kwa kuongeza sehemu ndogo ya (e) inayoanzisha Kituo cha
Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), kubainisha malengo ya kuanzishwa Kituo
na majukumu yake pamoja na kuweka masharti kuhusu uongozi na vyanzo
vya fedha za Kituo.
Amesema kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro kimeendelea kutekeleza
majukumu yake na kutokana na kutokutambuliwa kisheria kinashindwa
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ikiwemo kushindwa kuingia
mikataba ya kitaifa na kimatifa na hivyo kukosa fedha za kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.
Waziri Masauni ameongeza kuwa kituo kinashindwa kusimamia kwa karibu
masuala ya uuzaji na ununuzi wa viwango vya kaboni kwani hakitambuliki
kisheria na kwamba kimekuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais tangu
kuanzishwa kwake na hivyo kinategemewa kuendelea kuwa chini ya Ofisi hiyo
ili kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi zaidi hususan katika eneo la
mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni kwa ujumla wake.
Pia, Waziri Masauni amesema vifungu vya 30 na 31 vinapendekezwa
kurekebishwa kwa kuviongezea vitengo vya usimamizi wa mazingira
vinavyoanzishwa katika wizara na taasisi mbalimbali jukumu la kushughulikia
pia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wizara
za kisekta zinatekeleza masuala ya Mabadiliko ya tabianchi kikamilifu.
Ameongeza, Ibara ya 13 ya Muswada inapendekeza kuongeza kifungu cha
75A katika Sheria kwa lengo la kuimarisha mfumo wa kitaasisi wa kuratibu
masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambapo Kamati ya Taifa ya Ushauri wa
Mazingira itatambulika kama Kamati ya Taifa ya Mabadiliko ya Tabianchi.
Kwa upande wake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira
imeonesha kuridhsihwa na marekebisho madogo 11yaliyofanywa katika na
Serikali katika Muswada huo.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti Mhe. Jackson
Kiswaga, Mhe. Agnes Hokororo ili kukidhi matarajio ya Bunge, wananchi na
maudhui ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Kamati inaona kuwa
ipo haja kwa Serikali kuwasilisha Miswada ya Sheria mipya itakayowezesha
kutungwa kwa Sheria ya kulifanya Baraza la Taifa la Mazingira kuwa Mamlaka
pamoja na Sheria ya masuala ya Uchumi wa buluu.
Hivyo, baada ya hatua hiyo Naibu Spika Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema
baada ya Miswada hiyo kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inapelekwa kwa Rais ili iweze kusainiwa na kuwa Sheria kamili.