Chama cha ACT Wazalendo kimefanikiwa kushinda mapingamizi saba kati ya 13 yaliyowekwa na mawakili wa serikali katika kesi tulizozifungua za kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji uliofanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Kigoma, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Ndugu Yunus Luhovya, amesema mawakili wa chama wamepambana kwa nguvu na kufanikiwa kushinda mapingamizi saba hadi kufikia leo, huku mengine yakendelea kusikilizwa.
Ndugu Luhovya alionyesha masikitiko yake kwa serikali kwa kuzuia kusikilizwa kwa kesi za msingi kwa kuweka mapingamizi katika kesi zote za uchaguzi. Alisema kuwa mawakili wa serikali wanadai kuwa waliofungua kesi hizo hawakuwa wagombea halali, jambo ambalo si la kweli na linakusudia kuziondoa kesi hizo mahakamani kabla ya ushahidi kusikilizwa.
Aidha, Ndugu Luhovya alitoa wito kwa wanachama wa ACT Wazalendo wanaohudhuria mahakamani kuendelea kufika kwa ujasiri ili kujionea wenyewe jinsi haki inavyopatikana mahakamani.