Na Lucas Raphael, Tabora
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi ,Maliasili na Utalii imeipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kukamilisha mradi wa jengo la maktaba katika chuo cha Ardhi ,kampasi ya Tabora, mradi uliosimama takribani miaka kumi (10) iliyopita, na mradi huu hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.
Pongezi hizo zilitolewa jana mwenyekiti wa kamati hiyo Timotheo Mzava kwa niaba ya wabunge wa wajumbe wa Kamati hiyo .
Kamati ilifanya ziara ya siku moja mkoani hapa kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi wa jengo la maktaba lenye urefu wa ghorafa mbili.
Licha ya kutoa pongezi hizo kwa kuweza kukamilisha jengo hilo, pia aliitaka wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya makazi kuhakikisha inambana mkandarasi M/S Brave Engineering and Construction Co.Ltd ili kurejesha kiasi cha milioni 51 anachodaiwa kwa mujibu wa mkataba baada ya kushindwa kujenga mradi huu na kusababisha mkataba wake kuunjwa
Mzava alisema kwamba fedha hizo zikipatina zitumike kutatua changamoto mbalimbali katika chuo hicho, lakini pia Wizara ihakikishe jengo linaanza kutumika haraka pindi linapokamilika.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya kudumu wa bunge aliwataka wakandarasi wazawa wanaopewa kazi na serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa uhadilifu mkubwa, kwani Serikali inawapa kipaumbele ili kukuza uwezo wa kampuni hizi ziwe na ushindani wa Kimataifa.
Hata hivyo, Naibu waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Geofrery Pinda, alieleza kuwa amepokea maelekezo, maoni na ushauri wa Kamati na ameihakikishia kamati hiyo ya kudumu ya bunge kwamba, kama Wizara watahakiksha fedha hizo zinarejeshwa ili zitumike katika matumizi mengine chuoni hapo.
Aidha aliwahakikishia Wabunge wa Kamati hii ya kudumu kuwa jengo hili la Maktaba ujenzi wake utakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, na Wanachuo wataanza kutumia jengo hilo mwezi machi mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha aliendelea kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuupendelea Mkoa wa Tabora kwa miradi ya maendeleo na ameihakikishia Kamati kuwa Ofisi yake imepambana sana kuhakikisha kuwa miradi yote ya muda mrefu inakamilika ukiwamo mradi huu wa ujenzi wa maktaba.