Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) CPA. Sadock Mugendi (wa kwanza kushoto), Afisa Uhusiano ETDCO Bi. Samia Chande pamoja na Msimamizi wa Mradi Bw. Thobias Jackson wakikagua Mradi wa Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mkoa wa Tabora hadi Urambo.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) wakiwa katika picha ya pamoja na Meneja Mkuu wa ETDCO CPA. Sadock Mugendi wakati walipotembelea kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Wilaya ya Urambo.
Miundombinu ya Mradi wa Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mkoa wa Tabora hadi Urambo iliyojengwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO)
…….
Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) CPA. Sadock Mugendi amesema Mradi wa Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mkoa wa Tabora hadi Urambo unaotekelezwa ETDCO umefika asilimia 97 kumalizika.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, CPA. Mugendi amesema kuwa kwasasa wapo hatua za mwisho za ukaguzi, huku akieleza kuwa wanatarajia mpaka kufikia mwezi Februari, 2025 mwishoni mradi utakuawa umekamilika na kuunganishwa katika kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Wilaya ya Urambo.
CPA. Mugendi ameishukuru serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassan kupitia Wizara ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati Dkt. Doto Biteko katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili watanzania waweze kupata umeme wa uhakika wakati wote.
Naye Msimamizi wa Mradi Bw. Thobias Jackson, amesema kuwa wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mradi huo, hivyo amewataka wananchi wa Wilaya ya Urambo kuchangamkia fursa kwani wanakweenda kupata huduma ya umeme ya uhakika ukilinganisha na kipindi cha nyuma.
Wakizungumzia umuhimu wa mradi huo Wananchi wa Wilaya ya Urambo, wameishukuru serikali kwa kufanikisha mradi wa upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana unakwenda kuwa mkombozi wa maisha kwa kuwaletea maendeleo, kwani awali umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara.
“Ujio wa mradi huu katika Wilaya yetu imetusaidia katika kupata ajira na kuingiza kipato, mradi umetupa fursa ya ajira ndogo ndogo na kutusaidia kuendesha maisha” amesema Mkazi wa Wilaya ya Urambo Bw. Almasi Ramadhani.