*Awapongeza wananchi kwa kuwa na ukumbi wa kisasa
*Ampongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuboresha elimu nchini
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Bukombe hususan Kata ya Bulangwa kwa kuwa na ukumbi wa mzuri na wa kisasa utakaotumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii.
Rais Kikwete amesema hayo leo Februari 8, 2025 katika Kata ya Bulangwa, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita wakati akiweka jiwe la msingi katika jengo la ukumbi lililopo katika Shule ya Sekondari Bulangwa.
Akieleza kuhusu ukumbi huo, Rais Kikwete amesema kuwa Dkt. Biteko alifurahishwa na ukumbi wa Shule ya Sekondari Lugoba uliopo katika Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani ambao ulijengwa na Kampuni na MMsteel hivyo alizungumza na Kampuni hiyo na baadae ujenzi wa ukumbi wa Bulangwa ulianza.
“ Niwapongeze sana wananchi wa Bulangwa kwa kupata ukumbi mkubwa na wa kisasa, nikipata nafasi nitakuja tena kutembelea ukumbi huu,” amesema Rais Kikwete.
Aidha, amempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha na kuendeleza sekta ya elimu nchini.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais Kikwete kwa kushiriki tukio hilo ambalo linaambatana na Mkutano Mkuu Maalum wa Jimbo la Bukombe unaolenga kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Bukombe kuanzia mwaka 2020 – 2025.
Dkt. Biteko ametaja sababu ya kujenga ukumbi huo ni uwepo wa Shule ya Sekondari Bulangwa na Chuo cha VETA kinachoendelea kujengwa sambamba na uwepo wa taasisi mbalimbali za Serikali karibu na eneo hilo.
“ Tunakushukuru sana kwa kutusaidia kujenga ukumbi wa kisasa na tunakuomba siku moja uje kututembelea wakati ukumbi huu ukiwa umekamilika,” amesema Dkt. Biteko.
Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Sane Machembe amesema kuwa ujenzi wa ukumbi huo ulianza tarehe Mei 5, 2024 na unatarajiwa kukamilika Machi 30, 2025.
“ Ukumbi huu una uwezo wa kuhudumia watu 3,500 hadi 4,000 kwa wakati mmoja na utakuwa na manufaa makubwa kwa Shule hii na jamii mfano wanafunzi kuwa na sehemu nzuri na salama ya kukusanyika kwa pamoja wakati wowote,” ameeleza Mwalimu Mkuu huyo.
Ameongeza “ Utapunguza gharama za uendeshaji wa mikutano kwa kukodi miundombinu. Pia, utaongeza mapato ya shule kwa kukodisha kwa watu wanaotaka kufanya sherehe za harusi na mikutano.”
Sambamba na hayo ameishukuru Serikali na Mbunge wa Jimbo hilo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa jitihada zao za kuboresha miundombinu mbalimbali katika Jimbo hilo.