Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika kikao cha wakuu wa nchi za SADC na EAC kinachojadili mzozo wa kisiasa Mashariki mwa Congo DRC kikao hicho kinafanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.
Rais William Ruto wa Jamhuri ya Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akishiriki katika kikao hicho.
Rais Paul Kagame wa Rwanda akishiriki katika kikao hicho. Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Jamhuri ya Uganda akishiriki katika kikao hicho.
Rais Emerson Ndabuzo Mnangagwa wa Jamhuri ya Zimbabwe na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC.
Rais Hakainde Hichilema wa Jamhuri ya Zambia akishiriki katika kikao hicho kinachoendelea Ikulu jijini Dar es Salaam.
……………….
NA JOHN BUKUKU- IKULU MAGOGONI
Jua lilikuwa linawaka kwa utulivu jijini Dar es Salaam, huku upepo wa Bahari ya Hindi ukipuliza kwa upole kuelekea Ikulu ya Magogoni , kana kwamba ulikuwa ukijaribu ukiashiria uzito wa maamuzi yaliyokuwa yakifikiwa ndani ya ukumbi wa Jakaya Kikwete, ndani ya ukumbi huo, viongozi tisa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamekusanyika kwa lengo moja kuu: kuumaliza mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mgogoro ambao umedumu kwa zaidi ya miongo miwili.
Mwenyeji wa mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, akazungunza kwa utulivu na ujasiri. Sauti yake ilikuwa thabiti lakini yenye kugusa mioyo, ikionyesha uzito wa jukumu alilolibeba kama Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC- Organ.
“Hatupaswi kukaa kimya tunaposhuhudia mateso ya watu wa DRC,” alisema kwa msisitizo, macho yake yakiwatazama viongozi wenzake dani ya ukumbi huo. “Ni wajibu wetu, kama viongozi, kushughulikia changamoto hii. Tanzania itaendelea kutumia nguvu za kidiplomasia kuhakikisha tunaleta suluhu ya kudumu.”Maneno yake yalionekana kuleta kutafakari na uzito wa hali hiyo kwa viongozi wenzake
Rais William Ruto wa Kenya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliinuka kuzungumza. Sauti yake ilijaa hekima na matumaini. “Mgogoro huu hautamalizika kwa mtutu wa bunduki,” alisema. “Ni kupitia mazungumzo na ushirikiano wa kidiplomasia ndipo suluhu ya kudumu itapatikana. Mazungumzo si udhaifu; ni nguvu inayotuwezesha kuelewana.”
Ruto aliongeza, kwa kueleza jinsi mgogoro wa DRC ulivyoathiri mamilioni ya watu. Watoto walilazimishwa kuingia vitani, familia zilifurushwa, na maisha yasiyo na hatia yakapotea. “Tunapaswa kuchukua hatua sasa, kabla hali haijazidi kuwa mbaya,” alisisitiza.
Kisha, Rais Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Mwenyekiti wa SADC, alisimama. Akiongea kwa sauti nzito yenye mamlaka, alikumbusha hadhira jinsi umoja wa Afrika ulivyowakomboa kutoka minyororo ya ukoloni. “Tunaposhuhudia hali ya DRC, tunapaswa kukumbuka mshikamano na undugu wetu,” alisema. “Kama tulivyopigania uhuru wa Afrika, ni lazima tushirikiane kutatua changamoto za usalama barani mwetu.”
Kila kiongozi aliyezungumza alionyesha dhamira ya kweli ya kutafuta suluhu. Mazungumzo hayo yalikuwa ya kina, yakionyesha mshikamano wa kipekee baina ya jumuiya hizi mbili kubwa za kikanda.
Mkutano huu ulikuwa sio tu juhudi za kutafuta amani ya DRC, bali pia mwanzo wa kushirikiana kwa nguvu mpya barani Afrika. Dar es Salaam, mji wa amani, ulitoa fursa ya kuandika historia mpya ya mshikamano wa kanda hizi mbili.