Na Ashrack Miraji Fullshagwe Media
Mjumbe wa Timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid (MSLAC) Bi.Angelina Sampa amesema mwanamke ana haki ya kumiliki Ardhi na Mali nyingine na anayo haki ya kushirikishwa pale Mali ya familia inapouzwa.
Akitoa Elimu ya umiliki wa Ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Kirore Kata ya Myamba, Bi. Sampa ambaye pia ni Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Same alisema katika maeneo mengi wanaume wamekuwa wakiuza mali za familia bila kumshirikisha mke jambo ambalo sio sahihi kisheria.
“Wanaume lazima mtambue kuwa mke ana haki katika Mali za familia lakini watoto wa kiume na wa kike wapaswa kujulishwa iwapo mali inauzwa au kununuliwa kwani wao Sheria inawatambua kama wanufaika”alisema Sampa.
Alisema watoto wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea wanapaswa kushirikishwa kwenye maamuzi yote yanayohusu Mali za familia.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imetoa elimu na Msaada wa Kisheria kwenye Kata kumi za Wilaya ya Same.
Said Senkoro ni Mkazi wa Kijiji cha Kirore Kata ya Myamba ambaye amemshukuru Rais Samia kwa kuwafikishia Msaada wa Kisheria kwani wananchi walio wengi hawajui haki zao.
Kwa upande wake Bi.Sifaeli Togolani Mkazi wa Myamba amesema anaaamini kwa elimu iliyotolewa utasaidia wanaume kubadilika kwani wanaume wengi vijijini hawatambui kama mwanamke ana haki.