………….
Na Saidi Lufune – Dodoma
Chuo kikuu cha Dodoma kupiti Idara ya Historia na Akiolojia kimeendelea kuunga Mkono jitihada za Wizara ya Maliasili na Utalii katika kulinda na kuhifadhi urithi wa malikale na utamaduni wa kitanzania kupitia maonesho ya kabila la Wagogo ili kusaidia kurithisha urithi huo adhimu kwa jamii.
Hayo yamesemwa katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma na Mkuu wa Idara ya Sanaa na Taaluma za Habari Chuo Kikuu Dodoma, Dkt. Deograsia Ndunguru katika Maonesho ya kabila la Wagogo yaliyoshirikikisha wanafunzi wanaosomea masomo ya Urithi wa Utamaduni, Historia na Utalii kwa lengo la kuwajengea uwezo, ufanisi na weledi wa kutoa elimu kwa jamii juu ya kulinda na kuhifadhi urithi wa watanzania.
“Lengo la fani hizi katika chuo hiki, ni kuzalisha wataalamu wabobezi watakao hudumu katika kuendeleza na kuhifadhi urithi wetu malikale na kiutamaduni na kutumia rasilimali hizo kama zao la kiutalii ili kushamirisha uchumi wa nchi yetu kwa kuwa ndio maono na ndoto za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Amesema Ndunguru
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya mambo ya kale anayeshughulikia maendeleo ya Malikale na Makumbusho, Mwita William amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale itaendelea kushirikiana na chuo kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Idara ya Historia na Akiolojia ili kuongeza nguvu katika kulinda na kuhifadhi urithi wa Malikale, historia na tamaduni za makabila nchini kwa kuwa kufanya hivyo itasaidia kutanua wigo wa kuitangaza Tanzania
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi Taaluma ya Urithi wa Utamaduni na Uendeshaji wa Makumbusho Bi. Selina Banzi amewataka wanafunzi wanaosomea masomo ya Historia na Malikale kutumia ujuzi na maarifa wanaopata chuoni hapo kwa kutoa elimu kwa jamii inayowazunguuka katika kulinda na kuhifadhi urithi wa malikale na tamaduni za mtanzania ambayo itaongeza thamani kwa makabila yetu na Taifa kwa ujumla
Naye, Chifu Mazengo mtawala wa kimila kutoka katika jamii ya wagogo ametoa wito kwa jamii kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhifadhi urithi wa watanzani hasa katika kipindi hiki cha utandawazi unaoingiza tamaduni nyingi za kigeni ndani ya nchi ikiwemo lugha, mavazi, vyakula na mwenendo wa maisha
Itakumbukwa kuwa miongoni mwa malengo matano ya sera ya utamaduni ya mwaka 1997 nchini Tanzania ni kushirikisha shughuli za Utamaduni wa Taifa kuanzia shule za awali, Sekondari na elimu ya Juu na kuhakikisha mafunzo ya hayo yanaingizwa katika mitaala na muhtasari na kufundishwa shuleni na vyuoni