Na WAF, DODOMA
Serikali imeweka mpango wa utoaji wa ufadhili kwa madaktari Bingwa na Bobezi chini ya mwamvuli wa (Samia scholarship) utakaohusisha pia mafunzo ya madaktari wataojikita kwenye magonjwa ya wazee.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni jijini Dodoma Februari 7, 2025 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ambaye amesema kuwa mbali na kuendelea kuwasomesha madaktari wa magonjwa ya wazee, Serikali pia inahakikisha wataalam wa saikolojia na sosholojia wanajumuishwa kwenye mpango huo kwa maslahi mapana ya kuhudumia wazee.
“Mpango huo wa Serikali wa utoaji wa ufadhili kwa madaktari (scholarship) utahusisha pia mafunzo ya madaktari wanaotaka kujikita kwenye magonjwa ya wazee, ikiwa ni pamoja na masuala ya saikolojia na ustawi wa kijamii,” amefafanua Dkt. Mollel.