Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), alipowapokea na kuzungumza na Maafisa Usafirishaji wa Mkoa wa Dodoma, wakiwa ni wamiliki na madereva wa bodaboda na bajaji, mara baada ya kuwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Hafla hii ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi, inayofanyika kuanzia tarehe 6 hadi 8 Februari, 2025.
……….
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma.
Mfumo wa kielektroniki wa Anwani za makazi (NaPA) ambao una programu tumizi yaani ‘Application’ utasaidia kuboresha huduma za usafiri na usalama wa abiria na madereva ambapo kwa kutumia simu janja madereva wanaweza kupakua application hiyo itakayowarahisishia kumfikia mteja kwa haraka kwa kuwa mfumo huo ni wa utambuzi wa maeneo.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) Februari 7, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma katika maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi ambapo amezungumza na maafisa usafirishaji wa bodaboda na bajaji wa Mkoa wa Dodoma.
Waziri Silaa ameuzungumzia mfumo huo wa NaPA ulio chini ya Wizara yake kuwa ni mfumo unaotumia simu za kiganjani na abiria wanaweza kuita huduma ya usafiri kwa kuingiza anwani zao za makazi katika mfumo huo, na maafisa usafirishaji almaarufu kama madereva wanaweza kufika moja kwa moja kwenye maeneo yao.
“Anwani za Makazi ni muhimu kwa utoaji wa huduma bora za usafiri, kwani husaidia katika upatikanaji wa maeneo kwa urahisi na usahihi. hata kama ni mgeni na hauifahamu Dodoma, kwa kutumia mfumo huu wa NaPA utaweza kumfikia mteja kwa urahisi,”, alisisitiza Waziri Silaa.
Waziri Silaa ametoa rai kwa maafisa usafirishaji kuwa mabalozi wa Mfumo wa kielektroniki wa Anwani za Makazi kwa kuutangaza na kuutumia katika shughuli zao za kila siku ili kuboresha huduma kwa kuwa mfumo huu unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri nchini.
Akitoa salamu za Maafisa Usafirishaji, Mwenyekiti wa Umoja Madereva Pikipiki Dodoma (UMAPIDO), Bw. Marwa Chacha Nyagake, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita na Rais Samia kwa kufanikisha uundaji wa mfumo huo, akieleza kuwa faida zake zinaanza kuonekana katika kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo huduma za usafirishaji.