Na Farida Mangube, Kilosa – Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujikita zaidi katika biashara ya hewa ukaa, akisisitiza kuwa ni moja ya njia za mkakati za kujikomboa kiuchumi kuanzia ngazi ya vijiji hadi halmashauri.
Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Uvunaji Misitu kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Shaka alisema biashara ya hewa ukaa ni sekta yenye utajiri mkubwa, na mafanikio yake tayari yameanza kuonekana baada ya juhudi za awali zilizofanyika wilayani humo.
“Kwa majaribio tuliyofanya, tumeonyesha kuwa tunaweza kufanikisha biashara hii na kupiga hatua. Nina imani kuwa mtakwenda kuwa mfano bora wa kusimamia rasilimali za wilaya yetu,” alisema Shaka.
Aliongeza kuwa mafanikio haya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyewataka wananchi kutumia fursa ya biashara ya hewa ukaa kwa kutunza mazingira na misitu.
“Tunajivunia mafanikio haya na tumedhamiria kuhakikisha tunatekeleza maelekezo ya Rais. Asali ya hewa ukaa tumeanza kuionja Kilosa. Tupo tayari kuendelea kuhakikisha tunatunza rasilimali zetu kwa manufaa ya wote,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Shaka, Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kuzalisha tani 545,433 za hewa ukaa, zikitarajiwa kuingiza mapato ya Shilingi bilioni 1.17. Alieleza kuwa kijiji cha Malolo, Msiba na Mhenda vimeongoza kwa mafanikio makubwa katika uzalishaji huo kati ya mwaka 2023 hadi Februari 2024.
“Biashara ya hewa ukaa ni njia bora ya kupunguza umasikini na kuongeza mapato ya halmashauri. Kadri uwekezaji huu utakavyozidi kuimarika, tunaweza kuwa mfano wa mafanikio katika sekta hii,” alisema.
Hata hivyo, Shaka alipiga marufuku uvunaji na usafishaji wa mashamba kiholela, akisisitiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kufanya hivyo bila vibali halali.
“Vijiji, kwa kushirikiana na Halmashauri, boresheni sheria ndogo za usimamizi wa misitu na wekeni adhabu kali kwa yeyote atakayehusika na ukataji wa miti au uharibifu wa misitu kiholela,” alisisitiza.
Kwa mafanikio haya, wakazi wa Kilosa sasa wana fursa ya kuimarisha uchumi wao huku wakichangia katika juhudi za kulinda mazingira.