Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Majid Mwanga (wa tatu kutoka kushoto) akikagua Mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini ( ETDCO).
Msimamizi wa Mradi wa Usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Katavi, Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) Abdulazizi Ngozi (wa kwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Mhe. Majid Mwanga kuhusu maendeleo ya mradi huo.
Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wakiwa kazini wakitekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkoa wa Tabora hadi Katavi.
…………….
Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe. Mhe. Majid Mwanga amefurahishwa na utekezaji wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) ambapo kupitia mradi huo Wilaya ya Mlele inatarajiwa kuunganishwa na gridi ya Taifa.
Akizungumza wakati akikagua utekelezaji wa mradi huo wa Usafirishaji wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, wenye jumla ya kilometa 383 ambao umekamilika asilimia 100.
Mhe. Mwanga ameishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan pamoja na Wizara ya Nishati inayoongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati Dkt. Doto Biteko katika kuhakisha Mkoa wa Katavi unaunganishwa na grid ya Taifa ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika jambo ambalo litasaidia ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja.
Aidha, ameipongeza ETDCO kwa kutumia wazawa katika utekezaji wa mradi huo kwani vijana mbalimbali wa Wilaya ya Mlele pamoja na Mkoa wa Katavi wamepata fursa ya ajira.
Msimamizi wa Mradi wa Usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Katavi, Abdulazizi Ngozi amesema mradi huo upo hatua ya mwisho na hadi kufikia mwisho wa mwezi Februari, 2025 umeme katika Wilaya ya Mlele utakuwa umeunganishwa na gridi ya Taifa.
Naye Chifu Kayanda wa kabila la wakonongo, wakazi wa wilaya ya mlele, ameipongeza ETDCO kwa utekezaji wa mradi wa usafirishaji umeme kwa kuonesha umahiri mkubwa katika kutimiza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha Mkoa wa Katavi unaunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa.
Amesema kuwa shughuli za kiuchumi katika Wilaya Mlele na Mkoa wa Katavi kwa ujumla zinakwenda kuleta tija kwani kipato cha wananchi kitaongezeka.
Wakizungumzia mradi huo, Wananchi wa Wilaya ya Mlele, wameishukru serikali kwa kuwaletea gridi ya umeme ya Taifa katika Wilaya hiyo, kwani wanakwenda kuondokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kutokana uzalishaji mdogo wa umeme uliokuwepo awali.
ETDCO ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye shughuli za ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na kufanya matengenezo kwenye miundombinu ya umeme nchini Tanzania.