Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI imesema majaribio ya utoaji wa barua za utambulisho kwa njia ya kidijitali kwa kutumia mfumo wa anuani za makazi (NAPA) yameonesha mafanikio katika kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma za utambuzi.
Hayo yameelezwa leo Februari 6, 2025 na Naibu Waziri OR – TAMISEMI Dkt. Festo Dugange wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika uzinduzi wa wiki ya anuani za makazi kwa mwaka 2025 inayoenda sambamba na maonesho ya huduma mbalimbali zinazotolewa kupitia huduma ya mtandao kwa kutumia anuani za makazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Dugange mbali na mafanikio makubwa yaliyo onekana katika hatua za awali za majaribio, mfumo huo wa NAPA umesaidi katika utekelezaji wa jukumu la kutoa majina ya mitaa na kugeuka nyenzo muhimu zaidi inayorahisisha utambuzi wa makazi, utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali.
Kutokana na ufanisi huo, Dkt. Dugange amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwaruhusu, kuwahamasisha na kuwahimiza waratibu wa mfumo huo katika maeneo yao kushiriki mafunzo ya mara kwa mara yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kupitia mfumo wa NAPA, ili wawe msaada wa kuwawezesha wananchi kutambua anuani zao.
Kadhalika ameeleza kuwa OR – TAMISEMI itaweka mazingira ya kutoa msaada wa kiufundi pale inapohitajika wakati wote, ikiwa ni hatua ya kudhibiti changamoto zinazo weza kujitokeza.
Kwa upande wake waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa amepongeza ushirikiano uliopo baina ya wizara hizo mbili akieleza namna unavyorahisha utekelezaji wa mfumo huo wa anuani za makazi.
Maadhimisho ya wiki ya anuani za makazi kwa mwaka 2025 yamebebwa na kauli mbiu ya “Tambua na tumia anwani za makazi kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma”.