Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi Camilius Wambura, amemvisha cheo cha Sajenti Koplo Emmanuel Kisiri, Polisi Kata wa Ikoma, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara. Koplo Kisiri ametunukiwa cheo hicho kutokana na juhudi kubwa alizozionyesha katika utendaji kazi wake kwa kushirikiana na jamii anayohudumia na wadau mbalimbali.
Hafla hiyo fupi ilifanyika katika kiwanja cha Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Kamnyonge, Manispaa ya Musoma, na kuhudhuriwa na maofisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali kutoka mkoani humo.
Baada ya kumvisha cheo hicho, Kamanda Lutumo aliwataka askari wote kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata mafunzo waliyoyapata katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na kujituma.
“Kutokana na jitihada alizozionyesha Koplo Emmanuel Kisiri, ni dhahiri kuwa ana uwezo wa kuongoza, hivyo anastahili kutunukiwa cheo cha Sajenti,” alisema Kamanda Lutumo.
Kwa cheo hicho kipya, Sajenti Kisiri anatakiwa kuendelea kuimarisha mshikamano na jamii kwa kuhakikisha usalama na amani vinadumishwa katika kata yake na maeneo ya jirani.