Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mgombea Urais mteule kupitia Chama cha Mapinduzi CCM akiwa amenyanyua mkono pamoja na Dkt. Ali Hassan Mwinyi kulia Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM pamoja na Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi wakati walipotambulishwa rasmi kwa wanachama na wananchi kwenye sherehe za miaka 48 ya CCM zilizofanyika leo Fabruari 5, 2025 kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
………….
NA JOHN BUKUKU – DODOMA
Kelele za vifijo na nderemo zilihanikiza anga la Dodoma wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipoadhimisha miaka 48 tangu kuasisiwa kwake. Hafla hiyo haikuwa tu ya sherehe, bali pia ilibeba uzito wa historia mpya kwa chama hicho, ambapo viongozi wake wakuu walitambulishwa rasmi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Jukwaa lilipambwa kwa rangi za kijani na njano, huku wanachama na mashabiki waliofurika wakionyesha mshikamano wao kupitia nyimbo na kauli mbiu za chama. Katika hotuba yake ya kipekee, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisimama imara mbele ya umati huo, akitoa mwito wa mshikamano kwa wanachama wote.
“CCM tuna wanachama zaidi ya milioni 12,” alisema Dkt. Samia kwa sauti yenye kujiamini. “Tuna deni la kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.”
Kabla ya hotuba ya Dkt. Samia, CCM ilidhihirisha nguvu zake za kiuchumi kwa kuonyesha mabasi mapya, magari maalum kwa ajili ya wagombea urais Bara na Zanzibar, pikipiki, na baiskeli zitakazotumika wakati wa kampeni. Hili lilikuwa ni onyesho la ushindi wa kimkakati, linaloonyesha kuwa chama hicho si tu chama cha siasa bali pia chombo chenye mfumo imara wa kiutendaji.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alionyesha utayari wake wa kushirikiana na Dkt. Samia, akiahidi kuimarisha kampeni kwa lengo la kuhakikisha CCM inazidi kung’ara.
“Nitahakikisha tunapata ushindi wa kishindo na kuimarisha nguvu za chama chetu,” alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama waliokuwepo.
Naye Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, alitumia fursa hiyo kusisitiza mafanikio makubwa ambayo CCM imeyapata, akiwakumbusha wanachama umuhimu wa kuyaendeleza mafanikio hayo.
“Chama chetu kimeonyesha uongozi thabiti na mafanikio makubwa kwa wananchi, na tuna kila sababu ya kujivunia,” alisema Dkt. Mwinyi kwa kujiamini.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wassira, kwa upande wake, alitoa kauli ya uthibitisho kuwa hakuna chama kingine kinachoweza kushindana na CCM.
“Hakuna hati yoyote inayosema tulikubaliana na mtu yeyote kubaki madarakani. Ushindi wetu ni halali,” alisema Wassira huku akiongeza msisimko kwa wanachama waliofurika uwanjani.
Sherehe hizi za kihistoria zimeacha hisia za matumaini makubwa kwa wanachama wa CCM, huku chama hicho kikijiandaa kuingia katika uchaguzi mkuu kwa kishindo na kuendelea kushika hatamu za uongozi nchini.
Picha za matukio mbalimbali ya maadhimisho ya miaka 48 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliofanyika leo Februri 5, 2025 Mkoani Dodoma.