Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wanachama wa CCM kujivunia mafanikio makubwa ya chama hicho, huku akiwasihi kuwa mabalozi wa maendeleo katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi nchini.
Akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya CCM katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, tarehe 5 Februari 2025, Dkt. Mwinyi alisema mafanikio yaliyopatikana tangu kuasisiwa kwa CCM ni uthibitisho wa uimara na uthabiti wa chama hicho katika kutekeleza sera zake kwa maslahi ya Watanzania wote.
Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 umeonyesha dhamira ya kweli ya chama hicho kuwaletea wananchi maendeleo, huku akiwahimiza Wana-CCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. “Ili CCM iendelee kushika dola na kufanikisha maendeleo, kila mmoja wenu ahakikishe anashiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao,” alieleza.
Aidha, Dkt. Mwinyi alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake mahiri ambao umefanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika maadhimisho hayo, pia ilikumbukwa kuwa CCM kiliundwa tarehe 5 Februari 1977 kwa kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, tukio ambalo lilikuwa na historia ya kipekee katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Dkt. Mwinyi alihitimisha kwa kuwahimiza Wana-CCM kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mshikamano, kudumisha amani, na kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyofikiwa yanatetea heshima ya chama kwa kizazi cha sasa na kijacho.