Na. Anangisye Mwateba-Bungeni Dodoma
Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu (FWITC) kilichopo Wilayani Mafinga mkoani Iringa ambacho kiko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni fursa muhimu kwa vijana kupata maarifa ya kuongeza thamani mazao ya misitu hususan mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa anatoa majibu Bungeni baada ya swali lililoulizwa na Mhe. Deodatus Philip Mwanyika ambaye alitaka kujua Serikali itachukua hatua gani za kuhakikisha uvunaji wa rasilimali za misitu unazingatia uongezaji thamani.
Mhe. Kitandula alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya vijana 27 wa kozi ndefu na vijana 103 wa kozi fupi wamehitimu ambao hutumika kutoa mafunzo kwa wakulima wa miti katika mikoa hiyo.
“Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Mazao ya Mbao yaliyohandisiwa wa mwaka 2021 pamoja na Mpango Kazi wake wa mwaka (2021–2031). Mpango Mkakati huu umesaidia katika kuimarisha uzalishaji na biashara ya mazao ya misitu yaliyohandisiwa, ambapo hadi sasa kuna jumla ya viwanda 48 vinavyozalisha bidhaa ya venia katika Mikoa ya Iringa na Njombe na kati ya viwanda hivyo, viwanda 27 vipo katika jimbo la Njombe Mjini” aliongeza Mhe. Kitandula
Vilevile, Wizara imeandaa kanuni kupitia Tangazo la Serikali Na. 266 la tarehe 31 Machi ,2023 linalolenga kusimamia usafirishaji wa bidhaa na mazao ya misitu yanayoingia na yanayoenda nje ya nchi.
Aidha hadi kufikia Desemba, 2024 kiasi cha mita za ujazo 38,056 za bidhaa za misitu zilizoongezewa thamani (EWPs) zenye thamani ya USD 9,079,813 zilisafirishwa kwenda nje ya nchi.