Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili kwa watendaji wa Uboreshaji mkoa wa Tanga wakifanya mafunzo kwa vitendo ya namna ya kuendesha vifaa vya Biometriki (BVR) vitakavyotumika katika zoezi la uboreshaji Mkoani Tanga ambapo zoezi la Uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linataraji kuanza Februari 13 hadi 19, 2025. (Picha na INEC).
…………
Na Mwandishi wetu, Tanga na Pwani
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa ya Tanga na Pwani kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zake katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Asina Omari wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa TEHAMA Mkoani Pwani jana.
“Mnapaswa kutekeleza majukumu mliyopewa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kanuni zilizotungwa chini ya vipengele vya sheria hiyo vinavyohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”alisema Mhe. Jaji Asina.
Aidha, alitoa wito kwa watendaji hao kuhakikisha kuwa wanaendelea kutumia muda wao wa ziada kusoma na kupitia maelekezo yote waliyopewa ili kuongeza uelewa zaidi kuhusu wajibu na majukumu yao katika zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani” amesema Mhe. Jaji Asina.
Akifunga mafunzo kama hayo Mkoani Tanga nakuhusisha washiriki kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe, Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangira amewataka watendaji hao kutekeleza jukumu la kuhamasisha wananchi wa maeneo yao kushiriki kwenye uboreshaji kwa kushirikiana na wadau wengine wa uchaguzi.
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” alisema Mhe. Rwebangira.
Alisisitiza kuwa jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji, kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo mlizo nazo.
“Mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika shehia zote zilizopo katika mikoa yote mitatu ya Unguja. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika shehia zote” amesema Mhe. Magdalena.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa ya Tanga na Pwani umepangwa kufanyika kuanzia tarehe 13 hadi 19 Februari, 2025 ambapo vituo vitafunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni.