Na WAF, DODOMA
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema Tanzania imekuwa kituo muhimu cha matibabu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na nchi nyingine jirani, huku akitaja juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya.
Akichangia taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa mwaka 2024 iliyo wasishwa Bingeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Elibarick Kingu, leo Februari 04, 2025 Dkt. Mollel amesema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Rais Samia kutengeneza wasomi na wataalam wa afya kwa ajili ya miaka 100 ijayo.
Dkt. Mollel amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ya kisasa ya afya, ambayo imetengeneza mazingira bora kwa wananchi wa Tanzania na mataifa jirani kupata huduma za matibabu za kisasa.
Amefafanua kwamba uwekezaji huu umeifanya Tanzania kuwa kivutio kwa watu kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki, kuja kupata huduma.
“Kupitia mkakati wa Rais Samia, Tanzania sasa inashika nafasi ya kuwa pool ya matibabu kwa Kanda ya Afrika Mashariki, ambapo wananchi wa nchi jirani wanakuja kupata matibabu ya kisasa. ,” amesema Dkt. Mollel.
Pia, Dkt. Mollel ameongeza kuwa juhudi hizo hazilengi tu kutatua changamoto za afya nchini Tanzania, bali pia kuleta suluhu za afya kwa nchi za jirani,
Serikali ya Rais Samia imeongeza matumizi ya teknolojia ya habari katika sekta ya afya, na kuanzisha mifumo ya kisasa ya utoaji wa huduma, ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu vya kisasa. Huu ni mwanzo wa kuunda mazingira bora zaidi ya kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Mollel ametoa wito kwa Kamati ya Afya na wadau wote wa sekta ya afya kushirikiana ili kuhakikisha juhudi za kuboresha huduma za afya zinaendelea kufanikiwa na kwamba Tanzania inabaki kuwa kielelezo cha mafanikio katika sekta ya afya barani Afrika.