Na Fauzia Mussa
MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abasi Ali, amewahimiza wanawake kujiandikisha katika daftari la wapiga kura awamu ya pili litakapofika katika wilaya zao ili kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi.
Akizungumza na wanachama wa vikundi vya ushirika vya wanawake wa Shehia saba za Jimbo la Welezo katika Soko la Wajasiriamali Wadogo Makufuli, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Siti alisema kuwa licha ya kila mwananchi kuwa na haki ya kupiga na kupigiwa kura, kutokuwa na kitambulisho cha mpiga kura kunawanyima fursa hiyo muhimu.
Alibainisha kuwa uzoefu unaonyesha wanawake wengi husita kugombea nafasi za uongozi, hali inayowafanya kutoona umuhimu wa kujiandikisha, hivyo kujikosesha nafasi ya kuchagua viongozi wanaowafaa.
Aidha, aliwataka akina mama kuwahamasisha na kuwasimamia vijana wao waliotimiza umri wa kupiga kura kuhakikisha wanajiandikisha ili nao waweze kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa katiba.
“Tuhamasishane kwenda kujiandikisha ili tupate nafasi ya kupiga kura na kumchagua Dk. Hussein Ali Mwinyi aendelee kutuletea maendeleo zaidi na kutatua changamoto zetu,” alisema Siti.
Alisisitiza kuwa Rais Mwinyi ameleta maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa jinsia wala umri, hivyo ni muhimu kwa wanawake kuchukua hatua na kuhakikisha wanajiandikisha ili wasikose fursa ya kushiriki uchaguzi.
Kwa upande wao, wanawake walioshiriki kikao hicho waliahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kushiriki zoezi hilo na kuhakikisha kila mwenye sifa anajiandikisha.
Sheha wa Shehia ya Mtofaani, Rehema Ame Hatibu, aliwasihi akinamama kuwaongoza vijana wao waliotimiza umri wa miaka 18 kujiandikisha, akisisitiza kuwa zoezi hilo litafanyika Machi 1-3 katika Wilaya ya Magharibi ‘A’.
Naye Mratibu wa Shehia ya Welezo, Betha Mathew Lukanguzi, aliwakumbusha wananchi kuwa kila mmoja ana haki na wajibu wa kujiandikisha ikiwa amekidhi vigezo. Alisisitiza umuhimu wa kushiriki zoezi hilo ili kupata fursa ya kuchagua viongozi sahihi watakaoleta maendeleo kwa wananchi wote.
Zoezi la uandikishaji wapiga kura awamu ya pili lilianza Februari 1 katika Wilaya ya Micheweni na linatarajiwa kuendelea katika wilaya zote za Unguja na Pemba, likihitimishwa Machi 17 katika Wilaya ya Mjini.