Jeshi la Polisi Tanzania limeihakikishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha kazi zao zinafanyika kwa ufanisi, kwa kuwa majukumu yao yanategemeana kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi vya kielektroniki (printa) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa leseni katika ofisi za RPC, Meneja wa Mkoa wa Kikodi wa Temeke, Masau Malima, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu serikali mtandao (ICT).
“Tunaunga mkono kauli ya Rais kuhakikisha kuwa serikali nzima sasa inasomana. Kwa sasa, mtu akitoka Polisi hatahitaji kuja na karatasi TRA, kwani taarifa zitakuwa kwenye mifumo yetu na tutazihudumia moja kwa moja. Hata hivyo, Polisi wanahitaji kuwa na kumbukumbu zao, ndiyo maana tumewaletea printa ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao,” alisema Malima
Aidha, alieleza kuwa TRA ina imani kuwa vifaa hivyo vitachangia kuboresha utendaji kazi wao na kuongeza mapato kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, SACP John Malulu, alishukuru kwa kupatiwa vitendea kazi hivyo vya kielektroniki, akisema vitasaidia kuharakisha huduma za leseni kwa wananchi.
“Iwapo tulikuwa tunachelewa kuwapatia wananchi leseni, sasa tutaongeza kasi kwa sababu tuna vitendea kazi vitakavyorahisisha utendaji wetu,” alisema Kamanda Malulu.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi na TRA wanategemeana sana katika eneo la utoaji wa leseni hasa katika masuala yanayohusiana na vyombo vya moto.
“Mwananchi anaweza kuanzia Polisi, lakini mwisho wa siku, leseni itatolewa na TRA,” alifafanua.