Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Kitaifa Mkoani Arusha Machi 8, 2025.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akionesha sare itakayokutumia katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Badru Abdulnoor akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Kitaifa Mkoani Arusha Machi 8, 2025.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali pamoja na wadau mbalimbali nchini wanatarajiwa kuungana kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Kitaifa Machi 8, 2025 Mkoani Arusha, huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” iliyotokana na Kau limbiu ya Kimataifa ‘’For All Women and Girls. Equality. Rights. Empowerment’’ ambapo imelenga kuhamasisha jamii katika kukuza Usawa, Haki na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo February 3, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa kabla ya siku ya kilele ya maadhimisho siku ya wanawake duniani yataendelea kuadhimishwa katika ngazi ya Mikoa nchi nzima ili kuwa na ushiriki wa Wanawake wote na watanzania kwa ujumla.
Dkt. Gwajima amesema kuwa wakati wa wiki ya maadhimisho Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi na Makampuni zitatoa huduma mbalimbali kwa wananchi pamoja na kuonesha maonesho ya bidhaa za wajasiriamali.
“Naomba wananchi wote wajitokeza katika maeneo yetu kupata huduma na kununua bidhaa mbalimbali, maadhimisho yatahusisha makundi mbalimbali wakiwemo Wanawake, wanaume, vijana wa kiume na kike, wadau wa maendeleo ya wanawake nchini, viongozi wa Serikali, Kisiasa, Kidini na Asasi za Kiraia” amesema Dkt. Gwajima.
Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba sura ya kipekee kwani yanaambatana na miaka 30 ya utekelezaji wa azimio la ulingo wa Beijing, kwani mwaka 1995 ulifanyika mkutano wa kujadili hali ya wanawake Duniani uliofanyikia Beijing, China.
Dkt. Gwajima ameeleza kuwa katika mkutano huo yalifikiwa maazimio ambayo Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeendelea kutekeleza.
“Mataifa yatatumia maadhimisho haya kutathimini utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing ikiwa pamoja na kuweka mikakati endelevu ya utekelezaji” ameseama Dkt. Gwajima.
Amesema hivyo katika kufikia malengo katika maadhimisho haya watahakikisha yanabeba sura ya kitaifa na kushirikisha wadau wote katika ngazi zote.
Akizungumzia ratiba ya kuanzia kwa maadhisho haya, Dkt. Gwajima amesema kuwa Machi 1, 2025 Mikoa, Wilaya na Kata zote nchini zitafanya uzinduzi wa maadhimisho kwa kushirikisha wanawake na wadau wote katika maeneo yao.
“Uzinduzi huo utaambatana na jamii kutathimini utekelezaji wa maazimio ya Beijing na kuweka mwelekeo wa utekelezaji katika maeneo yao” amesema Dkt. Gwajima.
Amesema kuwa Machi 3- 6, 2025, kutafanyika makongamano ya kikanda kwenye kanda saba ambapo Mikoa itakayohusika ni Dar es salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Mbeya, Lindi pamoja na Kigoma.
Amesema kuwa makongamano haya yanatarajiwa kufunguliwa na viongozi wa ngazi ya Kitaifa kuanzia Februari 3-6, 2025 , huku akifafanua kuwa kuanzia Machi 5-8, 2025 kutakuwa na maonesho ya wanawake wajasiriamali, Taasisi za Umma na Binafsi na Makampuni yatakayofanyika Mkoani Arusha.
“Machi 8, 2025 umeandaliwa usiku maalum wa mwanamke Mkoani Arusha na wanawake takribani 1,500 watashiriki, na itakuwa kilele cha maadhimisho ambapo wananchi kwenye Mikoa yote wataungana kuadhimisha siku hiyo” amesema Dkt. Gwajima.
Katika hatua nyengine amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho haya, imeandaliwa sare maalum ya Kitaifa ambacho ni kitenge kwa ajili ya kuvaliwa siku ya kilele Machi 8 Machi, 2025.
Amesema kuwa sare hiyo itasambazwa Mikoa yote na itapatikana kwa kujinunulia ambapo bei ya kitenge kwa watakaonunua jumla ni shilingi 25,000 na shilingi 30,000 kwa rejareja kutegemeana na umbali wa mahali.
“Nitumie fursa hii kuwajulisha wanawake wote kuhusu sare hii ya aina yake, rai yangu kwa wanawake kuwa siku ya kilele itapendeza sana tukijitokeza kwa wingi tukiwa tumevaa sare hizo” amesema Dkt. Gwajima.