………….
NA BALTAZAR MASHAKA, NYAMAGANA
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Kata ya Mabatini, Wilaya ya Nyamagana,mkoani Mwanza,wameadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM kwa kupanda miti 245 katika taasisi za umma.
Hatua hiyo inaonesha ni jinsi gani jamii inavyojizatiti kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wilayani humo.
Akizungumza na gazeti hili leo wakati wa kupanda miti hiyo , Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mabatini, Paul Yomola,amesema katika madhimisho hayo wamemua kupanda miti ya matunda na vivuli katika shule ya Sekondari Mtoni,Shule za Msingi Mabatini A na B ili kulinda na kutunza mazingira,kurejesha uoto wa asili.
Pia,upandaji miti huo wameufanya ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,katika utunzaji wa mazingira nchini na amekuwa kinara wa kuhamasisha utunzaji wa mazingira Afrika.
“Kupanda miti 245 ni hatua nzuri ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira pia,inaendana na juhudi za Rais Dk.Samia, katika kuhamasisha Afrika kutunza mazingira ikizingatiwa mazingira ni kila kitu katika maisha ya binadamu,”amesema Yomola.
Hivyo, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,ni muhimu kuyalinda na kuyatunza yawe salama na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwani tusipoyalinda yatatuadhibu.
Amesistiza kuwa miti hiyo 245 iliyopandwa katika Shule Sekondari Mtoni na Shule za Msingi Mabatini A na B,jamii ihakikishe inaitunza ili kuboresho mazingira na uoto wa asili.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mabatini,amesema kuwa upandaji miti katika maeneo ya taasisi za umma, ni njia mojawapo ya kuboresha mazingira na kurejesha uoto wa asili, hatua ambayo ni nzuri kwani miti ya matunda na vivuli itasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha ustawi wa jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabatini Kusini, Hamisi Nassoro, amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayosumbua dunia kwa sasa, hivyo jamii ina jukumu la kushiriki kikamilifu katika upandaji miti na kulinda mazingira.
Pia,Ilani ya CCM imeendelea kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kupanda miti kama suluhisho la kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.