Mkuu wa Idara ya Fedha Maendeleo Benki Bw. Nolasco Charles akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025 jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Idara ya Biashara Maendeleo Benki Bw. Emmanuel Mwaya (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha Maendeleo Benki Bw. Nolasco Charles wakati wakizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025, Dar es Salaam
……………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Maendeleo Benki imefanikiwa kuweka historia ya kuendelea kupata faida kwa miaka 10 mfululizo baada ya kupata matokeo mzuri ya utendaji kazi kwa mwaka 2024 ukilinganisha na mwaka 2023.
Mafanikio yaliopatikana ni pamoja na faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 3.69 ukilinganisha na bilioni 2.63 ambapo sawa na ukuaji wa asilimia 40.
Faida baada ya kodi bilioni 2.83 ukilinganisha na bilioni 2.35 sawa na ukuaji wa asilimia 40, Jumla ya mapato yamefikia bilioni 23.31 ukilinganisha na bilioni 18.97 sawa na ukuaji wa asilimia 23, Mapato halisi yatokanayo na riba bilioni 10.84 ukilinganisha na bilioni 8.05 sawa na ukuaji wa asilimia 35, huku uwiano wa gharama kwa mapato ikifikia asilimia 61.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 3, 2025, Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Fedha Maendeleo Benki Bw. Nolasco Charles, amesema kuwa ukuaji wa mapato na faida ulichangiwa na nidhamu ya utekelezaji wa mpango mkakati, ushirika na wateja pamoja na kujitolea kwa wafanyakazi katika utendaji kazi.
Bw. Charles amesema kuwa baadhi ya vichocheo vilivyopelekea matokeo mazuri ni pamoja na kuimarisha kwa biashara ya mikopo ambapo ukuaji wa kitabu cha mikopo umefikia shilingi bilioni 88.78 kwa mwaka 2024 kutoka bilioni 74.09 kwa mwaka 2023, huku ubora wa kitabu ukiimarika kwa asilimia 4 kutoka mikopo chechefu ya asilimia 4.95 iliyorepotiwa mwaka 2023 mpaka kufikia asilimia 4.76 kwa mwaka 2024.
Amesema kuwa amana za wateja zimekua kwa asilimia 14 kutoka shilingi bilioni 90.79 kwa mwaka 2023 hadi kufikia shilingi bilioni 103.73 kwa mwaka 2024, huku mali za benki zikiimarika kutoka bilioni 124.69 na kufikia bilioni 150.56 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 21.
Pia jumla za mali za benki zimeongezeka kwa asilimia 15 na kufikia mtaji wa shilingi bilioni 21.94 ambao unatosha kuwa na benki ya kitaifa na kufungua matawi nchi nzima.
‘Benki inaendelea kurudisha faida kwa jamii kwani mwaka 2024 tulifanikiwa kutumia zaidi ya shilingi milioni 180 ikijumuisha tukio la mbio za hisani (Maendeleo Bank Marathon 2024) ambapo jumla ya milioni 140 zilipatikana kwa ajili ya ununuzi wa vifaa katika wodi ya watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini ya KCMC, Kilimanjaro na ujenzi wa kituo cha watoto waliozaliwa na changamoto ya ulemavu wa akili cha Mtoni, Dar es Salaam” amesema Bw. Charles.
Amefafanua kuwa kipaombele cha mwaka 2025 ni kuendeleza ukuaji wa benki kwa njia ya kidijitali kwa kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa benki na kuifanya benki kuwa ya kisasa kwa kufanya uwekezaji kwenye teknolojia.
Bw. Charles amesema kuwa wanatajia kuongeza mtaji wa benki kwa kufungua tawi moja kati ya Mkoa wa Arusha, Dodoma na Mwanza kutokana na taarifa za utafiti pamoja na kuboresha kitengo cha huduma kwa wateja katika matawi yote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wote.
’’Tunatarajia kuanzisha bidhaa bunifu, rafiki zinazoendana na mahitaji ya wateja, kwa kufanya haya tutaweza kufikia malengo yetu ya muda mrefu na mfupi ikiwemo kuongeza faida kwa mwaka kutoka shilingi bilioni 2.8 kwa mwaka 2024 na kufikia shilingi bilioni 4 kwa mwaka 2025” amesema Bw. Charles.