*Dkt. Samia Suluhu Hassan kielelezo cha kukuza usawa na uwezeshaji wanawake nchini.
*Serikali kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili nchini dhidi ya Wanawake.
*Wanaume mstari mbele katika kuhamasisha maendeleo na usawa wa Kijinsia.
Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Imeelezwa kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2025 yatakuwa kwa namna ya kipekee yakibeba sura ya kipekee kwa kuwa yanaambatana na miaka 30 ya utekelezaji wa Azimio la ulingo wa Beijing (1995).
Hayo yamebainika jijini Dar Es Salaam Februari 03, 2025 wakati wa Mkutano wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na waandishi wa Habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2025.
Waziri Dkt. Gwajima amesema, kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2025 kitafanyika Kitaifa Mkoani Arusha na awali, kilele hicho kitatanguliwa na maadhimisho katika ngazi ya Mikoa nchi nzima ili kuwa na ushiriki wa Wanawake na jamii kwa wingi zaidi ambapo, kwenye siku ya kilele, Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katika mkutano huo wa Beijing yalifikiwa maazimio ambayo Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeendelea kutekeleza. Mwaka huu ni wa thelathini (30) tangu utekelezaji ulipoanza, hivyo mataifa yatatumia maadhimisho haya kutathimini utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing ikiwa pamoja na kuweka mikakati endelevu ya utekelezaji” amesema Waziri Dkt. Gwajima
Ameongeza kuwa wiki ya maadhimisho hayo Wizara, Taasisi za Umma na Binafsi na Makampuni zitatoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Vilevile kutakuwa na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali mbalimbali hivyo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza katika maeneo yao kupata huduma na kununua bidhaa mbalimbali.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” ambayo imetokana na Kaulimbiu ya Kimataifa ‘’For All Women and Girls. Equality. Rights. Empowerment’’. Lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kukuza Usawa, Haki na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana na kwa kuzingatia kipindi hiki kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ili, wajiamini, wajiandae na wajitokeze kugombea nafasi za uongozi.
Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau imeandaa Sare maalum ya Kitaifa ambacho ni kitenge kwa ajili ya kuvaliwa siku ya kilele. Sare hiyo itasambazwa Mikoa yote na itapatikana kwa bei ya Sh. 25,000/= na haitazidi Sh. 30,000/= kwa rejareja kutegemeana na umbali wa mahali. Aidha, kabla ya kilele cha maadhimisho, mikoa itaadhimisha kwa Sare zao.
Amesisitiza Serikali kwa kutambua umuhimu wa siku hiyo inahimiza Wanawake na Wananchi kwa ujumla kujitokeza katika maadhimisho kwa kushiriki matukio yote kuanzia uzinduzi, maonesho na makongamano ili kuwa na maadhimisho yenye tija na mafanikio kwa ustawi na maendeleo ya Wanawake hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema maadhimisho ya Mwaka huu yatakuwa na muonekano wa kipekee hasa ikizingatiwa kuwa huadhimishwa kitaifa kila baada ya miaka mitano hivyo kutakuwa na mijadala, makongamono na huduma mbalimbali zitakazotolewa na elimu juu ya masuala ya Uwezeshaji Wanawake na usawa wa Kijinsia.
Akijibu hoja mbalimbali za Waandishi wa Habari Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Badru Abdulnoor amesema, Serikali imeamua kufanya Maadhimisho hayo kitaifa mkoani Arusha ili kupaza sauti katika jamii ya Mkoa huo na Mikoa jirani kuachana na mila zisizofaa zinazorudisha nyuma Wanawake na Watoto wa kike na kuhamamisha Wanaume kuunga mkono juhudi za Serikali na Wadau kuhusu Usawa wa Kijinsia nchini.