Timu ya Simba SC imerejea kileleni mwa ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji, Tabora United katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa leo Februari 2, 2025 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Winga wa Simba SC Mkongo Elia Mpanzu Kibisawala amefanikiwa kuisaidia timu yake kupata ushindi baada ya kuwa chachu ya upatikanaji wa mabao matatu, mawili yakifungwa na mshambuliaji Mcameroon Leonel Christian Ateba dakika ya 12 na 34, huku bao la tatu likifungwa na Shomari Salum Kapombe.

Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 43 na kurejea kileleni ikiwazidi pointi moja mabigwa watetezi Yanga SC baada ya wote kucheza mechi 16.

Tabora United kwa upande wao wanabaki na pointi zao 25 za mechi 16 wakiwa nafasi tano katika msimamo wa ligi.