Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameweka msisitizo juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya CCM na Prosperity Party (PP), chama tawala cha Ethiopia, katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Prosperity Party uliofanyika Addis Ababa mnamo Januari 31, 2025, Balozi Nchimbi alieleza kuwa urafiki wa vyama hivyo viwili umejengwa juu ya misingi imara ya kisiasa iliyowekwa na waasisi wa mataifa haya mawili. Alisisitiza kuwa kizazi cha sasa cha viongozi kina jukumu la kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu kwa manufaa ya wananchi.
“Kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunatoa pongezi kwa Prosperity Party chini ya uongozi wa Rais wake, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed. Uongozi wake madhubuti umewezesha Ethiopia kupiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,” alisema Balozi Nchimbi.
Aliongeza kuwa kupitia uhusiano wa vyama hivyo viwili, ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Ethiopia utazidi kuimarika, huku akisisitiza kuwa CCM itaendelea kushirikiana na PP na Serikali ya Ethiopia kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wananchi wa mataifa hayo mawili.
“Serikali ya Tanzania, inayoongozwa na CCM, itaendelea kushirikiana na Prosperity Party na Serikali ya Ethiopia ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanawafikia wananchi wa pande zote mbili,” alihitimisha Balozi Nchimbi.