Ashrack Miraji Fullshagwe Media
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Same limepitisha kiasi cha shilingi bilioni 63.420 kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kimaendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Bajeti hiyo imeidhinishwa katika kikao maalum cha baraza la madiwani kilichofanyika januari 31 kwa ajili ya kujadili na kupitisha mpango wa matumizi ya fedha kwa mwaka ujao wa fedha.
Akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Same Mhe. Yusto Mpande amesema bajeti hiyo imelenga kuboresha na kuimarisha sekta mbalimbali za kimaendeleo ndani ya wilaya ya Same ili kuimarisha ustawi wa wananchi wa Same.
Pia mwenyekiti huyo amewaomba watendaji pamoja na madiwani kuwa kipaumbele katika kuhakikisha mapato yanapatikana ili bajeti hiyo iweze kutimiza malengo ya kutekeleza miradi kwenye maeneo yao.
“Madiwani, watendaji pamoja na viongozi wote mliopo karibu na wananchi mna jukumu la kuhakikisha mapato yanapatikana ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa miradi ambayo tumepitisha bajeti hiyo leo’ amesema Mhe. Yusto
Katika bajeti hiyo imeweka kipaumbele kwenye umaliziaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyoishia kwenye maboma ikiwemo ya majengo ya shule, majengo ya miradi ya afya pamoja na mengineyo ili walengwa waweze kunufaika nayo.
Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Same Upendo Wera amepongeza namna bajeti hiyo ilivyowasilishwa na kuwaomba madiwani pamoja na watendaji kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato kutokana na uwepo wa mahitaji mengi zaidi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Damal James ambaye ni diwani wa kata ya Makanya amesema kuwa bajeti hiyo imelenga zaidi kwenye miradi inayoigusa jamii moja kwa moja ikiwemo elimu, afya na usafirishaji huku akiwasisitiza wananchi kushiriki katika shughuli za utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.
“Tunawashukuru sana wananchi wa same, wadau wa maendeleo na viongozi wetu, tunawaomba waendelee kujitoa kwa moyo kwenye kuunga mkono juhudi nza serikali katika maendeleo, wenye uwezo wa kuchangia chochote kwenye miradi yetu tunawaomba wafanye hivyo ili iweze kukamilika kwa wakati na iwanufaishe wananchi wetu wa wilaya ya Same” amesema Diwani Damal.
Hata hivyo baadhi ya madiwani wamepongeza mchakato wa uandaaji wa bajeti hiyo ambayo imegusa maeneo muhimu na kushauri kuwa baadhi ya miradi ina uchakavu na kuomba iweze kufanyiwa ukarabati