Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Janeth Elias Mahawanga, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)
……..
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi, utoaji wa risiti za mauzo na ununuzi wa bidhaa na huduma ikiwemo ya kutoa elimu ya kodi.
Mhe. Chande ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Janeth Elias Mahawanga aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti.
Mhe. Chande alisema kuwa elimu ya kodi inatolewa kwa njia ya redio, runinga, mitandao ya kijamii, makongamano, maonesho ya biashara ya kitaifa, kimataifa na semina.
Alisema kuwa Serikali inawatembelea wafanyabiashara katika maeneo yao mlango kwa mlango kutoa elimu inayoainisha wajibu wa mlipakodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wajibu wa TRA kwa mlipakodi kupitia Mkataba wa Huduma kwa Mlipakodi (Taxpayers’ Service Charter).
“Tumeanzisha huduma za bure ikiwemo namba za simu za bure zinazowezesha walipakodi kuwasiliana na Ofisi za TRA na tumeanzisha ofisi zinazotembea (mobile tax offices) ambazo zitatumika kama ofisi kamili kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi kwa umma na kusajili walipakodi wapya”, alieleza Mhe. Chande.
Akieleza kuhusu kuboresha Mfumo wa kutoa risiti, Mhe. Chande alisema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya mlipa kodi na kudhibiti mapato ya Serikali kwa kuweka msisitizo wa kuhakikisha mifumo yote inasomana na kuwa rafiki kwa mlipa kodi.
Alisema kuwa kwa sasa Serikali kupitia TRA imeweka mazingira wezeshi ambayo yanamsaidia mfanyabiashara kutoa risiti ya kielektroniki- EFD ambayo kwa njia ya simu ya mkononi na hiyo ndio sababu ya mapato kuongezeka siku hadi siku.