Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akieleza utayari wa Serikali wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya sekta ya elimu na afya ikiwemo kukamilisha kwa maboma yaliyojengwa na wananchi, bungeni jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha).
………
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza zoezi la kutoa fedha kwa ajili ya vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo na ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa na wananchi.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akitoa majibu ya nyongeza baada ya maswali ya wabunge kuhusu fedha za ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishaji wa maboma ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi katika sekta ya afya na elimu.
“Tuko katika hatua ya mwisho kuanza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya elimu na vituo vya afya msingi itakayokwenda sambamba na ukamilishaji wa maboma ambayo yamejengwa kwa nguvu ya wananchi”, alisema Dkt. Nchemba.
Awali Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, alilieleza Bunge kuwa Serikali itatoa kiasi cha shilingi milioni 250 kwa kila jimbo kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya kutolea huduma za afya msingi, zikiwemo Zahanati.
Alisema kuwa Wabunge walijaza fomu za kuainisha maeneo ya kimkakati katika majimbo yao ili kujenga vituo vya afya kupitia fedha kutoka Serikali Kuu na mapato ya ndani kutoka Halmashauri.
Aidha, alizihimiza Halmashauri kupitia mapato ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu hiyo muhimu ya afya msingi.