Katibu wa CCM ilaya ya Ilemela, Hassan Millanga, akisisitiza jambo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilemela, leo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela,Renatus Mulunga (wa pili kutoka kulia),leo akizindua mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kukata utepe,kulia ni Naibu Meya,Manusura Said.Mitambo hiyo imegharimu bilini 1.6.
Mstahiki Meya wa Ilemela, Renatus Mulunga, akizungumza na waandishi wa habari leo, baadaya kuzindua mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara.Kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi.
Mstahiki Meya wa Ilemela,Renatus Mulunga,akiendesha moja ya mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya barabaraleo, ikiwa ni ishara ya kuizindua.
Baadhi ya Madiwani wakiwa katika picha ya pamoja na Mstahiki Meya wa Ilemela, Renatus Mulunga(wa tatu kutoka kushoto), leo baada ya kuzindua mitambo ya ujenzi wa miundominu ya barabara, iliyogharimu sh.bilioni 1.4.Picha zote na Baltazar Mashaka
………….
NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Ilemela,kimewapongeza na kuwaagiza Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,kufanya mikutano ya hadhara kueleza mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita.
Ponezi na agizo hilo limetolewa leo, na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Millanga, wakati akitoa salamu za Chama katika Baraza la Madiwani hao,huku akionesha kuridhishwa na madiwani kufanya vikao vyake vya robo ya pili na kuzipatia ufumbuzi kero na changamoto mbalimbali zinazokabili wananchi.
Amesema madiwani hao wamefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano kwa kuhamasisha maendeleo katika manispaa hiyo na kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupigiwa kura nyingi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.
“Kwa kazi kubwa mliyofanya niwapongeze,lakini sasa kila mmoja atumie fursa iliyobaki kufanya mikutano ya hadhara kueleza yale yaliyofanywa ya maendeleo yaliyoletwa na serikali,hii italeta heshima kwa CCM na wananchi wetu,”amesema Millanga.
Pia,ameipongeza manispaa hiyo kwa kununua vifaa na mitambo ya ujenzi wa barabara,ifungwe mfumo wa utambuzi na ufuatiliaji kufahamu mitambo hiyo inafanya kazi eneo gani lakini pia kuepuka wizi wa vipuri.
“Niwapongeze kwa ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,,matumizi na usalama wa vyombo hivi, Mkurugenzi ufanyika utaratibu wa kuvifungia vifaa vya GPS kufahamu vinafanya kazi wapi.Hii itasaidia kudhibiti hujuma na wizi wa vipuri,”amesema Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Ilemela na kuongeza;
“Huwezi kuwatenganisha madiwani wa CCM na Chama.Niipongeze Manispaa ya Ilemela kwa kufunga mfumo wa ulipaji na ukusanyaji wa mapato katika ofisi ya Kata ya Nyamanoro.”
Aidha,amewashauri watalaamu wa manispaa hiyo kufunga mifumo hiyo katika kata zote 19 ili kupunguza msongamano na kurahisha ulipaji wa kodi za serikali kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela,Renatus Mulunga,amewaongoza madiwani kuzindua mitambo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyonunuliwa kwa gharama ya sh.bilioni 1.4 za mapato ya ndani.
“Manispaa ya Ilemela imeonesha njia na kuwa ya kwanza kununua mitambo yake ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Mwanza.Tuendelee kufanya kazi katika kata zetu kwani maendeleo hayaji kama mvua, yanatafutwa,hivyo tumieni akili na maarifa kuyatafuta,”amesema.
Kwa mujibu wa Mstahiki Meya,mitambo hiyo ambayo ni lori moja,greda na kijiko itafanya kazi ya kuchonga na kukarabati barabara kwa siku mbili katika kila kata.
Ametumia fursa hiyo kufafanua kuwa ili shughuli za maendeleo zitekelezwe kwa ufanisi ni lazima kasi ya ukusanyaji mapato iongezeke, hivyo madiwani wahakikishe wanashirikiana na watendaji katika ukusanyaji wa mapato.
“Ukusanyaji wa mapato si jambo la kisiasa na maendeleo si ya CCM wala CUF ni ya wananchi wote,wapiga kura wetu wanatutegemea sana katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi,miradi yote tuliyoahidi kutekeleza haiwezi kukamilika kama hatutakusanya mapato vizuri,” amesema Mulunga.
Amewataka viongozi na watendaji wa manispaa hiyo kuhamasisha jamii kuwapeleka watoto shule waanze kidato cha kwanza bila vikwazo,ili uwezekezaji uliofanywa na serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya elimu uwe na tija pia,wataalamu wabadilishe mitaizamo na kuacha kujenga madarasa mtawanyo bali wajenge mfumo wa ghorofa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela,Egidy Teulas amesema manispaa hiyo inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo tofauti.