Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, akizungumza na
Prof. Gerald Eisenkopf, wa Chuo Kikuu cha Vechta nchini Ujerumani, alipotembelea
ofisini kwake.
Prof. Gerald Eisenkopf akizungumza wakati alipokutana na Makamu Mkuu wa Chuo
Prof. Kusiluka. Pembeni ya Gerald ni Prof. Ismail Ismail, Mkuu wa Ndaki ya Biashara na
Uchumi.
Prof.Kusiluka akimkabidhi zawadi ya ukumbusho Prof. Gerald Eisenkopf
Prof. Kusiluka(katikati), Dkt. David Mrisho wa Chuo Kikuu cha SAUT (kulia), Prof.
Gerald Eisenkopf (kushoto), wakiwa akiwa na ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dodoma
katika picha ya pamoja.
Hapa wakibadilishana mawasiliano na kuagana, baada ya kumaliza mazungumzo.
Kushoto ni Prof. Razack Lokina ( Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma) na katikakati
ni Prof. Albinus Tenge ( Mkuu wa Ndaki ya Insia).
………..
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amekutana na
kufanya mazungumzo na Prof. Gerald Eisenkopf, wa Chuo Kikuu cha Vechta nchini
Ujerumani ambacho kimekuwa na ushirikiano na UDOM toka mwaka 2023, kupitia
Idara Sosholojia na Anthropolojia iliyopo Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii (CHSS).
Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Chuo Kikuu cha
Dodoma, Jengo la Benjamin Mkapa, Dodoma, leo tarehe 30 Januari 2025. Katika
Mazumgumzo hayo Prof. Kusiluka ameeleza malengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma ya
kuongeza wigo wa ushirikiano na Chuo hicho na hasa kwenye maeneo yanayohusu
Uchumi wa Afya kwa kuanzisha programu za Shahada za Uzamili kwa ushirikiano na
Chuo hicho.
“Katika kuhakikisha Chuo chetu kinatekeleza kwa vitendo Ukimataifaji, tumejizatiti
kuhakikisha tunaanzisha shahada za pamoja na washirika wetu, usimamizi wa pamoja
wa Tasnifu, pamoja na kuanzisha programu za masafa “ on line” ili watanzania wengi
waweze kunufaika na Chuo chao kwa kupata mafunzo popote walipo” alisisitiza
Aidha amewataka wataalamu wanapofanya mapitio ya Mkataba wa Makubalino na
Chuo Kikuu cha Vechta, kupanua wigo kwa kuhakikisha Idara zingine zilizopo ndani ya
Chuo hicho zinanufaika na ushirikiano huo.
Kwa upande wake Prof. Gerald Eisenkopf, ameshukuru kwa utayari wa UDOM
kushirikiana na Chuo cha Vechta, na kwamba suala la ufudishaji kwa njia ya mtandao
kwa sasa haliepukiki na Chuo chake kiko tayari kuendelea kushirikiana na Chuo Kikuu
cha Dodoma.
Aidha, amesema wako tayari kuanzisha pogramu za pamoja kwa kutumia
wataalamu walionao, kuendelea kubadilishana wataalamu, kuanzisha usimamizi wa
pamoja wa Tasnifu pamoja na kufanya utafiti na kwamba daima watakuwa tayari kutoa
msaada kadiri utakavyohitajika.
Kupitia ushirikiano huo tayari mfanyakazi mmoja amepata udhamini wa masomo ya
Shahada ya Uzamivu kupitia mpango wa mafunzo. Maeneo mengine yaliyoazimiwa
kuboreshwa ni kuandika miradi ya pamoja ya utafiti pamoja na Kujenga uwezo wa tafiti
zinazofanywa na wanafunzi wa Shahada za Uzamivu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Razack
Lokina, RASI wa Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, Prof. Albinus Tenge, RASI wa
Ndani ya Biashara na Uchumi Prof. Ismail Ismail, Dkt. David Mrisho wa Chuo Kikuu cha
SAUT ambao nao wana ushirikiano na Chuo hicho, pamoja na wakuu wa Idara ambazo
Chuo Kikuu cha Vechta, kinatekeleza makubaliano ya ushirikiano.