NA BALTAZAR MASHAKA, ILEMELA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela,imepitisha bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bilioni 84.3 kwa mwaka wa fedha 2025/26,kukiwa na ongezeko la asilimia tisa za mapato ya ndani.
Akiwasilisha rasimu ya makadirio hayo katika Baraza la Madiwami,kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,leo,Mchumi wa Manispaa hiyo,Helbert Bilia amesema
katika mwaka wa fedha 2025/26,Manispaa ya Ilemela inaomba kuidhinishwa sh. bilioni 84.3 za maendeleo,mishahara na matumizi ya kawaida.
Amesema kati hizo sh. bilioni 9.5 ni za maendeleo kutoka serikali kuu,mapato ya ndani sh.bilioni 15.0 ambazo,mishahara sh.bilioni 55.7 na sh.biliponi 4.3 za matumizi ya kawaida.
Bilia amesema katika makisio ya bajeti ya mapato ya sh.bilioni 15.0 kutoka vyanzo vya ndani, sh.bilioni 3.4 zitaumika kutatua changamoto za sekta za elimu,afya na huduma za jamii kwa kukamilisha miradi viporo.
“Miradi yote viporo 150 iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kila kata, tutaikamilisha katika bajeti ya mwaka huu,sekta ya elimu msingi miradi 66, sekondari 63, utawala 17,afya na maeneo meingine,”amesema mchumi huyo wa Ilemela.
Amesema asilimia 76 ya eneo la Manispaa ya Ilemela ni maji,hivyo itanunuliwa boti itakayotumika kudhibiti ukwepaji kodi (ushuru) ziwani,huku bajeti ikitarajiwa kuboresha maeneo ya mialo ikiwemo ya Igombe,Kirumba na Kayenze, ili kuzifanya rasilimali za mazao ya majini ziwe endelevu.
“Tunatarajia kununua bori ya doria kudhibiti ukwepaji kodi ziwani ambako kwa makusudi watu hawataki kulipa ushuru ama kodi ya serikali.Hivyo, msimu huu shule mpya za sh.milioni 400 zitajengwa,tumenunua pia vitendea kazi vya ujenzi kwa kodi zinazolipwa na wananchi kuhakikisha tunatekeleza miradi ya kijamii,”amesema Bilia.
Akizungumzia uwekezaji amesema serikali imetoa fursa kupitia mfumo wa uwekezaji kwa ubia,hivyo kuna maeneo sita wameyatangaza ambayo ni vyanzo vitakavyosaidia kuongeza mapato ya manispaa na kuiwezesha kujiendesha.
“Eneo la Buzuruga ilipokuwa stendi ya mabadi ni muhimu,tunataka kujenga kitega uchumi cha kibishahara ambacho kitabadilisha mandhari ya hapo pia,nyumba za watumishi zitaboreshwa ili kuongeza mapato ya halmashauri,”amesema Bilia.
Baadhi ya madiwani wamepongeza rasimu hiyo ya bajeti kuwa ya mfano kwani haijawahi kugusa kata,sekta zote na wananchi,hivyo ikitekelezwa kwa weledi wananchi watakuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kuufanya uchaguzi mkuu ujao kuwa bora.
“Ni bajeti ya kimkakati tunapoelekea katika uchaguzi mkuu,imegusa kila sekta, kata na wananchi ni maeneo machache yanahitaji maboresho.Ikisimamiwa vizuri huko kwa wananchi wetu, ilani itakuwa imetekelezwa kwa viwango,”amesema Dede Swila, Diwani wa Shibula (CCM).
Diwani wa Buswelu,Sarah Ng’hwani amesema bajeti hiyo inakidhi vigezo, kazi iliyobaki ni kwa madiwani kuwaambia wananchi kazi ya kuleta maendeleo inayofanywa na serikali yao ambapo alishauri zahanati ya Pasiansi ijengewe uzio kutokana na umuhimu wake.
Diwani wa Kirumba,Wessa Juma Wessa ‘Mzee wa Majabali’ amempongeza mchumi wa Ilemela (Helbert Bilia) akisema wasione timu inamng’ang’ania mchezaji,basi Ilemela imepata mchumi mweledi ambaye amekuwa chachu ya maendeleo na roho ya uchumi wa manispaa hiyo.