Na WAF, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Seif Shekalaghe leo Januari 28, 2025 ameshiriki katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Ufaransa na Hospitali ya Aga Khan kuhusu uimarishaji wa huduma za saratani katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo iliyofanyika hospitali ya Aga Khan, Serikali ya Ufaransa iliwakilishwa na Balozi wake nchini Mhe. Anne Sophie Av’e, ambaye ameeleza hisia zake kuhusu namna ugonjwa huo unavyoathiri wanawake nchini na kusababisha changamoto katika familia.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa baada ya wa awali ambao ulidumu kwa miaka minne kumalizika muda wake.
Hata hivyo amefurahishwa kwa uanzishwaji wa kituo cha matibabu ya Saratani katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road ambacho ni tumaini kwa akina mama wengi wenye matatizo ya Saratani.
Akitoa salamu za Wizara ya Afya katika halfa hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa msaada inayoutoa kwa Hospitali ya Aga Khan na kwa Tanzania kwa ujumla na ameahidi Serikali kuendelea kushirikiana na hospitali hiyo katika kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.
Aidha, Katibu Mkuu ameitaka Hospitali ya Aga Khan pamoja huduma inazozitoa kwa wananchi ni vema pia kusaidia katika kuwajengea uwezo watumishi wa afya ili waweze kubaini dalili za saratani mapema na kutoa matatibu mapema au rufaa, kushirikisha jamii katika kutoa elimu kuhusu saratani ili waweze kufika vituoni mapema na kufanyiwa vipimo.
Pia ametaja maeneo mengine kuwa ni kusaidia utafiti katika eneo la saratani ili kubaini sababu za changamoto kwa lengo la kuwa na majawabu ya kudumu na ushirikiano kati yake na taasisi za Serikali ili kuimarisha ubora wa huduma kwa wagonjwa wa Saratani.
Dkt Seif Shekalaghe amesema kwamba kuhudhuria kwake katika hafla hiyo ya kusaini hati ya Makubaliano ni ishara kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya afya katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo za Saratani.