Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 katika mtaa wa Kangaye kata ya Nyakato wilayani Ilemela uliokuwa ukihusisha wananchi wa mtaa huo na mwekezaji
Hassan Issa Shekila ni Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi kata ya Nyakato ambapo amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa juhudi zake katika kumaliza mgogoro huo na kufanikisha zoezi la upimaji kwaajili ya kumilikisha wananchi viwanja vyao baada ya kuishi maisha ya wasi wasi kwa muda mrefu
‘.. Kiukweli tunampongeza Mbunge wetu, ni msikivu na amekuwa na Sisi kwa kipindi chote cha mgogoro huu, Kila tulipomuendea alitusikiliza na mara ya mwisho alikuja katika eneo lenye mgogoro na kutoa maelekezo yaliyosaidia Leo tuweze kupimiwa viwanja vyetu ..’ Alisema
Aidha Ndugu Shekila amewataka wananchi wenzake kukumbuka fadhila za Mbunge huyo na kuhakikisha wanaendelea kushirikiana nae na kumuombea kwa Mungu Ili aweze kusimamia na kutekeleza shughuli za maendeleo za kila siku akishirikiana na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Nae Afisa upimaji wa ardhi manispaa ya Ilemela Ndugu Chacha Samson amefafanua kuwa yeye akishirikiana na wataalam wengine wanaendesha zoezi la kubaini mipaka na kupima eneo la mtaa wa Kangaye kata ya Nyakato ili kubaini vipande vya ardhi vya kila mwananchi ili mpango wa matumizi bora ya ardhi uweze kufuatwa na baadae wananchi wanaohusika waweze kumilikishwa viwanja hivyo
Kwa upande wake Bi Nusra Yahya Ramadhan ambae ni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo wanaokabiliwa na mgogoro huo wa ardhi amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kujitoa na kuhakikisha anashirikiana na Serikali kusaidia wananchi hao ambapo alifanya mikutano ya hadhara na kuagiza wataalam wa manispaa ya Ilemela kumaliza mara moja mgogoro huo kwa kushirikisha ofisi yake
Manispaa ya Ilemela ilikuwa ikikabiliwa na migogoro mbalimbali ya ardhi ikiwemo uwanja wa ndege na wananchi wa kata ya Shibula, polisi Kigoto na wananchi wa kata ya Kirumba, Magereza na wananchi wa Ilalila, jeshi la wananachi na wananachi wa Lukube na mpaka sasa chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Mbunge Dkt Angeline Mabula migogoro hiyo imeweza kupata ufumbuzi na kutatuliwa huku migogoro michache baina ya wananchi kwa wananchi ikiendelea kumalizwa kwa asilimia kubwa