Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile kulia wakati akikabidhiwa msaada na afisa Mwandamizi kutoka Wakala wa meli Tanzania TASAC
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupokea msaada huo.
………………
Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa: Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile ametoa onyo kali kwa baadhi ya wananchi yakiwemo makundi na taasisi zinazochangisha michango kufuatia maafa yaliyotokea Nankanga bonde la ziwa Rukwa.
Chirukile ametoa kauli hiyo Januari 29,2025 wakati akikabidhi vifaa tiba katika zahanati ya Nankanga.
Amemtaka katibu tawala wilaya ya Sumbawanga Gabriel Masinga kufuatilia taasisi iliyohusika kuchangisha michango kufuatia maafa yaliyotokea bonde la ziwa Rukwa.
“Wapo wananchi wachache ambao wanatumia maafa haya kujinufaisha kwa kuchangisha michango ili kuwasaidia wahanga wa maafa haya nawataka waache mara moja kwani ofisi yangu haijatoa kibali kwa watu kuchangisha “amesema Chirukile.
Pia mkuu huyo wa wilaya amesema juhudi zinaendelea za kutafuta mwili wa mvuvi mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngosha na kuwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki.
Wakala wa meli Tanzania TASAC ambao ndio waliotoa vifaa tiba ili kuwasaidia wananchi wa Nankanga amesema wametoa msaada wa vifaa mbali mbali pamoja na vitendanishi kwa lengo la kuwasaidia wananchi hao waliokumbwa na maafa.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya sh mill 10.vimetolewa katika zahanati 3 za Nankanga,Mtowisa na Milepa ambazo ni kata zilizokumbwa na maafa hayo.
Vifaa hivyo ni pamoja na magodoro 45,mashuka 200 ndoo 20 pamoja na vifaa tiba.
Awali akizungumza mbele ya mgeni rasmi afisa Mwandamizi wa Wakala wa meli Tanzania TASAC David Chiragi amesema vifaa hivyo vimetolewa kwa lengo la kuwasaidia watu waliopata madhira kutokana na dhoruba iliyotokea bonde la ziwa Rukwa.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Evalista Lugando ameishukuru TASAC kwa msaada huo kwani hapo awali walikuwa wanajifungulia chini.
“Tunaishukuru TASAC kwa msaada huo kwani hapo awali tulikuwa tunajifungulia chini kutokana na kukosa magodoro na ndoo kwa ajili ya kuhifadhia maji ilikuwa ni changamoto kubwa” amesema.
Maafa hayo yalitokea Januari 23, 2025 majira ya saa tatu asubuhi katika bonde la ziwa Rukwa ambapo wavuvi 550 waliingia ziwani kwa lengo la kufanya shughuli za uvuvi wa Kila siku lakini walikumbwa na dhoruba kubwa katika ziwa hilo.
Baada ya timu ya uokoaji kufika kutoka jeshi la zimamoto na uokoaji wakishirikiana na wananchi walifanikiwa kuwaokoa wavuvi 540 wakiwa hai huku wavuvi wengine tisa wakipoteza maisha.
Mpaka kufikia mchana wa leo Januari 29,2025 Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji Chacha Mchaka amesema wanaendelea kuutafuta mwili wa mvuvi mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngosha.