Katibu Tawala wa Wilaya ya Buhigwe, Mh. Utefta Mahega, amewataka watumishi wa umma wilayani humo kuzingatia demokrasia na utawala bora ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Akizungumza leo, Januari 29, 2025, katika mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Mh. Mahega alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya serikali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Ndugu George Emmanuel Mbilinyi, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwasihi watumishi kuyatumia kuboresha utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Mratibu wa mafunzo hayo, Bi. Joyce Mushi, amesema lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo viongozi wa serikali za mitaa ili waweze kutatua changamoto na malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na demokrasia.
Aidha, ameishukuru serikali kwa kufanikisha mafunzo hayo na kupongeza watumishi kwa kushiriki kikamilifu hadi mwisho wa programu, akisisitiza kuwa juhudi hizi zinaendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao, wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe wamesema wamejifunza mada mbalimbali zitakazowasaidia kuboresha utendaji kazi wao, hususan katika suala la ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya serikali.