Na Fauzia Mussa
Wazee na walezi wametakiwa kuwahamasisha vijana wao waliofikia umri wa kupiga kura kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura wakati awamu ya pili ya zoezi hilo itakapofanyika.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Vijana Zanzibar, Mohammed Kassim Mohammed, maarufu kama Prince Eddycool, wakati wa mkutano na wazee na vijana wa Shehia ya Miwani, Wilaya ya Kati Unguja. Hafla hiyo pia ilikuwa ya kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa hatua zake za kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo kijiji cha Miwani.
Prince Eddycool alisema kuwa uzoefu unaonyesha kwamba wananchi wengi, hususan vijana, wanatamani kuendelea kuongozwa na Rais Mwinyi. Hata hivyo, alisisitiza kwamba bila ya kujiandikisha na kushiriki katika upigaji kura, malengo hayo hayawezi kutimia.
“Ili tumrejeshe tena Dk. Mwinyi atuongoze kwa miaka mitano mingine, ni lazima vijana na wananchi wote kwa ujumla tuhakikishe tunajiandikisha. Bila kufanya hivyo, hatutaweza kushiriki katika zoezi la kupiga kura,” alikumbusha.
Aliongeza kuwa vijana wengi wakiandikishwa katika daftari hilo, itakuwa ni mtaji mkubwa wa kuhakikisha Rais Mwinyi anarejea madarakani na kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.
Kwa upande wao, vijana wa Shehia ya Miwani waliahidi kushirikiana na kuhamasishana ili kuhakikisha idadi kubwa ya vijana wanajiandikisha na kupiga kura kwa lengo la kumrejesha Rais Mwinyi kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Mustafa Zahor Mansour, mmoja wa vijana hao, alisema kuwa maendeleo yaliyofanikishwa na Rais Mwinyi ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake yamewapa matumaini makubwa.
“Kwa mambo aliyofanya Rais Mwinyi ndani ya miaka minne, ni sawa na miaka mia moja. Hakika hatuna cha kumlipa zaidi ya kumpa kura zetu nyingi kwa kumrejesha madarakani,” alisema Mustafa.
Naye Mwajuma Said Kaupenda, Katibu wa CCM Tawi la Miwani, alisisitiza kuwa kazi nzuri inayofanywa na Rais Mwinyi haihitaji mjadala, na kumrejesha madarakani ni jambo la msingi kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
“Rais wetu ametufanyia mambo makubwa. Tunamshukuru kwa namna ya kipekee, na tunajua wema pekee tunaoweza kumlipa ni kumpa kura nyingi kwenye sanduku la kura,” alisema Mwajuma.
Kwa mujibu wa taarifa, zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika Wilaya ya Kati Unguja linatarajiwa kuanza Machi 8 na kumalizika Machi 10 mwaka huu.