Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Riziki pembe Juma amewataka waratibu wa wanawake na watoto na Masheha kuhakikisha wanasimamia ipasavyo suala zima la uanzishwaji wa Majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika shehia zao, ili maalengo ya kianzishwa kwake yaweze kufikiwa.
Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati alipofungua Mafunzo ya Uanzishwaji wa Majukwaa ya uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kwa Masheha na waratibu wa wanawake na watoto wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Micheweeni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema lengo la kuanzishwa majukwaa hayo ni kuwaweka pamoja wanawake kishehia na kuanzisha vikundi vya ushirika na kuvisajili pamoja na kuzungumzia fursa mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuondokana na utegemezi.
Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanzia Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika kuona wanamnyanyua mwanamke kiuchumi.
Amesema viongozi hao wamekuwa wakitoa fursa nyingi katika kuwasaidia wanawake kuodokana na utegemezi lakini haziwafikiwi ipasavyo, hivyo amesema imani yake ni kuwa kuanzishwa kwa majukwaa hayo yatasaidia kuwafikia fursa hizo kama zilivyokusudiwa.
” Katika shehia zenu mnajuana, hivyo ni vyema kuhakikisha mnashirikiana na mnaweka mikakati imara katika kuwasimamisha wanawake walipo ndani ya shehia zenu ili muweze kufaidika na fursa zitakazotolewa na sio kuwaingiza wasiohusika na shehia” amesisitiza Mhe.Riziki
Aidha amewashukuru kwa uwepo wao na kuwataka kuendelea kupambana na masuala yote ya kijamii ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao.
Akiwasilisha muongozo wa majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika ngazi ya Shehia, Afisa Jinsia kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto bwana Mohammed Jabir amesema kumeonekana kuna baadhi ya vikundi kuwepo kwa tatizo la kupigwa dane dane juu ya kupata usajili wa kikundi chao, hali ambayo inarudisha nyuma juhudi za ukuaji wa uchumi.
Wakitoa michango yao baadhi ya waratibu na masheha wamesema kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wana vikundi kutokuwa na elimu ya kutojua kusoma wala kuandika, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya kutosha ili malengo ya kuanzishwa majukwaa hayo yaweze kufikia.
Hata hivyo wamesema wapo tayari kuwaelimisha wanashehia na jamii zilizowazunguka juu ya umuhimu wa uanzishaji wa majukwaa hayo katika shehia zao ili waweze kufaidika na fursa mbakimbali.