Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) ni miongoni mwa taasisi za Serikali zinazoshiriki maonesho katika mkutano wa Nishati unaohusisha wakuu wa Nchi za Africa (Africa Energy Summit) ambapo jana umefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko na kuendelea leo tarehe 28, 2025 katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliowakutanisha wakuu wa nchi zaidi ya 25 barani Afrika, wawakilishi wa wakuu wa nchi na mashirika ya kimataifa ambapo Tanzania ni Nchi mwenyeji umejikita kujadili na kuimarisha sekta ya nishati, jitihada za upatikanaji wa umeme, kuboresha miundombinu ya nishati, na kutafuta suluhu za changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo.
Vilevile mkutano huo unalenga kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwenye sekta ya nishati, vyanzo mbadala kama vile jua, upepo, na gesi asilia.
NCAA inashiriki mkutano huo kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani na nje ya hifadhi ya Ngorongoro na kuelezea wageni shughuli za utalii zinazofanyika ndani ya hifadhi ikiwemo utalii wa picha, utalii wa utamaduni na mambo kale, utalii wa miamba (Geo tourism), Utalii wa anga (Astro tourism) kupitia Kimondo cha Mbozi, utalii wa kutembea (walking Safaris), utalii wa kupanda milima (hiking), utalii wa puto (Balloon Safaris) pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo Ngorongoro.
Aidha NCAA kupitia mkutano huo inatumia fursa kutoa mualiko kwa wageni mbalimbali wanaoshiriki kutembelea eneo la Ngorongoro hususan eneo la Ndutu ambapo msimu huu ni mahsusi kwa Nyumbu wanaohama ambao wanaendelea kuzailiana kwa wingi katika eneo la Ndutu.