Meya wa jiji la Arusha Maxmilian Iranghe na Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,John Kayombo wakikata utepe ishara ya uzinduzi wa mtambo mmoja na malori mawili kwa ajili ya ujenzi wa barabara zilizogharimu.shs 1.7 bilioni fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranghe akizungumza katika uzinduzi wa mitambo hiyo mkoani Arusha leo
Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,John Kayombo akizungumza katika uzinduzi huo mkoani Arusha.
………..
Happy Lazaro, Arusha
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranghe amezindua mtambo mmoja na malori mawili kwa ajili ya ujenzi wa barabara zilizogharimu.shs 1.7 bilioni fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha.
Akizungumza katika halfa ya uzinduzi huo uliofanyika leo mjini hapa, Iranghe amesema kuwa,jiji hilo liliamua kuweka bajeti ya kununua mitambo hiyo ambayo ni greda la kuchonga barabara pamoja na malori makubwa mawili kwa kuwa barabara nyingi ndani ya Jiji hilo ni mbovu na haziko kwenye mpango wa kutengenezwa na Tarura.
Amesema barabara zinazotengenezwa na Tarura ni zile zenye upana wa mita 12 huku barabara nyingi zinazokatiza mitaani zina upana wa mita 4 hadi 8 na hivyo kuzifanya zisiweze kupitika na kuleta kero kwa wananchi.
“Nawaomba sana madiwani pamoja na watendaji wa mitaa ndani ya jiji hilo kuhakikisha wanaelekeza wananchi kutofanya shughuli za ujenzi ndani ya hifadhi za barabara zinazokatiza kwenye mitaa yao ili kuwapa urahisi wajenzi pindi watakapopita kuchonga barabara mitaani kwao.”amesema Meya .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,John Kayombo amesema kuwa,hakutakuwepo na wananchi watakaolalamika kuhusu ubovu wa barabara tena kufuatia jiji kununua mitambo mipya ya kuchonga barabara hizo.
“Napenda kuwaeleza wananchi wa jiji la Arusha kuwa tatizo kubwa la barabara mbovu na korofi ndani ya Jiji la Arusha linaenda kumalizwa kabisa baada ya Halmashauri ya Jiji hilo kununua mitambo yake binafsi ya kuchonga barabara za mitaa yenye thamani ya bilioni 1.7.”amesema Kayombo.
Kayombo amesema mitambo hiyo imenunuliwa kwa fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Jiji la Arusha ambapo jumla ya bilioni 2 zilitengwa huku bilioni 300 zilizosalia zikigawanywa kwa kila kata ili kununulia vifusi.
“ Mitambo hii tumenunua kwa fedha zetu za ndani, hivyo ni jukumu la kila mkazi wa Arusha kujivunia uwepo wa mitambo hii, na hivyo napenda kutoa rai kwa kila mwananchi wa jiji la Arusha kuwa mlinzi wa mitambo hii,”amesema.
Amesema katika ununuzi huo, greda la kuchonga barabara limegharimu zaidi ya bilioni 1.3, huku malori makubwa mawili yamenunuliwa kwa zaidi ya milioni 400 ambapo jumla ya mitaa 154 katika kata 25 zinatarajiwa kufikiwa.
Naye Mhandisi wa jiji la Arusha ,Jacob Mwakyambiki amesema kuwa,baada ya kukabithiwa mitambo hiyo kazi ndo inaenda kuanza rasmi ambapo wataanzia na kata zilizopo pembezoni kwa ajili ya kukarabati barabara zote korofi na hatimaye kuweza kuondokana na changamoto hiyo.