Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina, akizungumza katika Mkutano wa Nishati Afrika ulioanza leo Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Julius Nyerere JNICC.
DAR ES SALAAM
Na. Mwandishi Wetu
Tanzania imeendelea kujidhihirisha kama kinara wa uongozi bora barani Afrika katika kuboresha upatikanaji wa nishati, hasa kwa kufanikisha kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,318, hatua inayotoa somo kwa mataifa mengine.
Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina, akizungumza katika Mkutano wa Nishati Afrika ulioanza leo Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam, ameisifu Tanzania kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa umeme unakuwa chachu ya maendeleo vijijini.
“Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa uwekezaji madhubuti katika miundombinu ya nishati. Nafasi hii ni fursa ya kumpongeza Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia juhudi hizi muhimu za maendeleo zinazoinufaisha jamii za vijijini,” alisema Dkt. Adesina.
Kwa kuzingatia umuhimu wa nishati ya umeme katika kuchochea maendeleo, Mkutano wa Nishati Afrika unalenga kuweka mkazo katika kuwaunganisha Waafrika milioni 300, hasa wale wanaoishi chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara, na nishati ya uhakika ifikapo mwaka 2030. Dkt. Adesina alisisitiza uwazi, uwajibikaji, na ushirikiano wa kimkakati kama nguzo za kufanikisha azma hiyo.
Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia, Mhe. Dkt. Situmbeko Musokotwane, ameishukuru Tanzania kwa msaada wake katika kuiuzia umeme, akisema kwamba ushirikiano huo umekuwa mkombozi kwa Zambia ambayo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa nishati.
“Tunatoa shukrani zetu kwa Tanzania kwa kutuuzia umeme, hatua inayosaidia kupunguza changamoto za nishati nchini kwetu. Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano wa kikanda,” alisema Dkt. Musokotwane.
Mkutano wa Nishati Afrika, unaofanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, unawakutanisha viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika, wadau wa maendeleo, na wataalamu wa sekta ya nishati. Malengo makuu ni kuweka mikakati ya pamoja, kushirikiana maarifa, na kuhakikisha Waafrika wengi zaidi wanapata nishati bora na salama kwa maendeleo endelevu.
Kupitia mkutano huu, Tanzania inaendelea kuwa mfano wa usimamizi mzuri wa rasilimali na utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wake, huku ikiimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya nishati.