DAR ES SALAAM
NA JOHN BBUKUKU
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameongoza juhudi mpya za kikanda kwa kuhimiza mshikamano wa nchi za Afrika katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati endelevu na nafuu kwa kila mwananchi ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza leo Januari 27, 2025, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nishati wa Nchi za Afrika jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko alibainisha kuwa mkutano huu ni fursa muhimu kwa bara la Afrika kuimarisha mikakati ya kuongeza upatikanaji wa umeme na matumizi ya nishati safi.
“Tuna jukumu la pamoja kuhakikisha tunafanikisha lengo la kuwafikishia umeme wa uhakika watu milioni 300 katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo mwaka 2030,” alisema Dkt. Biteko.
Aliendelea kusisitiza kuwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya viwanda, sekta ya madini, na huduma za kijamii, akihimiza nchi za Afrika kuongeza juhudi katika kuboresha miundombinu ya nishati.
Dkt. Biteko pia aliweka msisitizo juu ya matumizi ya nishati safi kwa kupikia kama sehemu ya malengo ya mkutano huo. “Ni lazima tutumie nafasi hii kuhakikisha jamii zetu zinapata fursa ya kutumia nishati safi ili kulinda afya na mazingira yetu,” alisema.
Mkutano huu ni juhudi za pamoja zinazoongozwa na Wakuu wa Nchi za Afrika, kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Dunia, na wadau wa maendeleo, ili kukabiliana na changamoto ya nishati inayowakabili Waafrika milioni 600 ambao bado hawajafikiwa na umeme.
Kwa ujumla, mkutano huu unalenga kuweka msingi wa Afrika yenye nishati endelevu, inayoaminika, na yenye gharama nafuu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.